Ripoti ya Benki ya Dunia.
9 Machi 2009Taarifa hiyo imetolewa jana na Benki ya dunia kabla ya kufanyika kwa mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa kundi la nchi 20 zilizoendelea kiviwanda pamoja na Wakuu wa Benki kuu, utakaofanyika Machi 14.
Kwa mujibu wa Benki hiyo ya Dunia, Biashara duniani inaelekea kupungua haraka, katika kipindi cha miaka 80 na athari zake zimezikumba sana nchi za Asia Mashariki.
Makadirio ya kiuchumi yamekuwa hayana matarajio mema zaidi kushinda ilivyokadiriwa na Shirika la Fedha Duniani -IMF-, ambalo mwezi Januari lilikadiria ukuaji wa asilimia 0.5.
Benki ya Dunia, imeonya kuwa katika hali hii ya mgogoro wa kiuchumi duniani, nchi zinazoendelea zitakabiliwa na ukosefu mkubwa wa fedha kwa kiasi kisichopungua dola bilioni 270 na kwamba kiwango hicho kinaweza kuzidi kufikia kiasi cha dola bilioni 700 kwa mwaka huu peke yake.
Mabenki binafsi yanayotoa mikopo yameyaacha masoko ya fedha katika nchi zinazoendelea.
Aidha Benki ya Dunia imesema, nchi tatu kati ya nne masikini zinaukosefu wa rasilimali katika kupambana na umasikini unaoongezeka katika kipindi hiki cha mgogoro wa kiuchumi duniani na kwamba Mashirika ya Fedha ya Kimataifa peke yake hayataweza kusaidia nchi hizo changa wakati wa mgogoro huu.
Mkuu wa Benki ya Dunia Robert Zoellick amesema ili kumaliza mgogoro huu wa uchumi duniani, ni muhimu juhudi zichukuliwe katika kupata suluhisho na kuzuia janga la kiuchumi katika nchi zinazoendelea.
Bwana Zoellick ametoa wito katika kuwekeza ili kuinua hali ya maisha ya jamii, miundombinu pamoja na viwanda vidogo na vya wastani ili kutoa nafasi za ajira kwa ajili ya kuzuia machafuko ya kijamii na kisiasa.
Benki ya Dunia imesema upungufu mkubwa katika hazina ya serikali za nchi tajiri inaweza kuchangia zaidi kukosa kupata mikopo kwa nchi changa.
Nchi zote zinazoendelea ambazo zinaweza kuchukua mikopo katika kipindi hiki cha mgogoro wa kichumi, zinaweza kulipa gharama zaidi.
Ripoti ya Benki ya Dunia imeonesha kwamba nchi 94 zinazoendelea kati ya 116 zimeonesha ukuaji mdogo wa kiuchumi.