1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Baraza la haki za binaadamu la Umoja wa mataifa yaishutumu Israel

23 Septemba 2010

Yasema kuvamiwa msafara wa meli za misaada kuelekea Gaza lilikuwa kosa.

https://p.dw.com/p/PKKP
Meli ya Mavi Marmara ship, iliovamiwa na makomando wa Israel Mei 31 mwaka huu.Picha: AP

Baraza la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu limetoa ripoti yake inayoeleza kuwa wanajeshi wa Israel walikiuka sheria za kimataifa, wakati wakati walipouvamia msafara wa meli zilizokuwa na misaada kwa wakaazi wakipalestina katika ukanda wa Gaza mwezi Mei. Itakumbukwa raia wanane wa Uturuki na Mmarekani mmoja mwenye asili ya Kituruki waliuawa pale wanajeshi wa Israel walipofyatua risasi wakati wa uvamizi huo.

Ripoti hiyo inasema kulikuwa na " ushahidi wa kutosha kwamba hatua ya wanajeshi wa Israel ilikiuka sheria za kimataiafa," kwa sababu kitendo cha jeshi la Israel kilikuwa ni mauaji ya kukusudia, mateso au uovu dhidi ya binaadamu, ambapo ambayo kwa kulingana na mkataba wa nne wa Geneva ni uhalifu.

Israel imeukataa utafiti huo, huku taarifa ya wizara yake ya mambo ya nchi za nje ikisema Baraza la haki za binaadamu lilikua na upendeleo na mtazamo mkali dhidi ya Israel na ndiyo maana ilikataa kushirikiana nalo katika uchunguzi huo. Israel kwa upande wake inafanya uchunguzi wake yenyewe.

Ripoti hiyo iliotolewa mjini Geneva ni tafauti na ile ilioamriwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa mjini New York, baada ya tukio la tarehe 31 Mei kwenye eneo la bahari nje ya mwambao wa ukanda wa Gaza, ambapo raia wanane wa Uturuki na Mamarekani mmoja mwenye asili ya Kituruki waliuawa.

Jopo la watu wanne lililoundwa na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, limekuwa likifanya uchunguzi mwengine tafauti na wa baraza la haki za binaadamu la umoja huo mjini Geneva na katika jopo hilo pia kuna wawakilishi wa Israel na Uturuki, na lilianza kazi yake tarehe 15 mwezi huu. Hadi sasa Umoja wa mataifa haujatoa maelezo yoyote juu ya pale zilipofikia shughuli za jopo hilo,

katika ripoti yake ya kurasa 56 hata hivyo, kwa upande wake baraza la haki za binaadamu la umoja wa mataifa, limesema hatua ya majeshi ya Israel wakati wa uvamizi wa meli ya "Mavi Marmara," iliokua sehemu ya msafara wa meli kuelekea Gaza ilikuwa moja kwa moja ukiukaji wa sheria za bahari za kimataifa na wa haki za binaadamu.

Israel iliitetea hatua hiyo ikisema ilihitajika kama njia moja wapo ya kuzuwia uingizaji silaha huko Gaza, eneo linalotawaliwa na chama cha msimamo mkali cha Hamas. Uchunguzi wa ripoti hiyo ulitokana na kazi iliopewa ujumbe wa utafiti na baraza la haki za binaadamu la Umoja wa mataifa. Walihojiwa mashahidi 100 mjini Geneva, London, Istanbul na Amman,lakini ombi la jopo la utafiti la baraza hilo kutaka kuwahoji Waisraili lilikataliwa na Israel.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman (dpa)

Mhariri :Josephat Charo