Ripoti: Usafiri wa anga ulikuwa shwari 2017
2 Januari 2018Mtandao wa Usalama wa Anga(ASN) umefanya utafiti na kubaini kuwa, mwaka 2017, ulikuwa mwaka salama kwa usafiri wa anga. Usafiri wa anga haukuwa na ajali yoyote iliyosababisha vifo katika ndege za abiria za biashara kwa mwaka jana. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mbili zinazojitegemea, zilizotolewa mwanzoni mwa huu 2018.
Kampuni ya ushauri wa usafiri wa anga ya Kijerumani, To70 na Mtandao wa Usalama wa Usafiri wa anga(ASN) walithibitisha kuwa hakukuwa na ajali mbaya ya ndege za abiria kwa mwaka 2017. ``Mwaka uliopita 2017, ulikuwa mwaka salama kwa usafiri wa anga`` Adrian Young wa To70 aliliambia Shirika la Habari la Reuters.
Kwa upande wake Rais wa mtandao ASN; Harro Ranter, alisema kwa wastani, tangu mwaka1997, idadi ya ajali za usafiri wa anga, imepungua kwa kasi.
Kwa kiasi kikubwa, alishukuru juhudi za kusimamia usalama zinazofanywa na Taasisi za kimataifa za mashirika ya usafiri wa anga, ikiwamo ICAO; IATA; na Flight Safety Foundation na kiwanda cha usafiri wa anga.
Vifo vinavyotokana na ajali za ndege, duniani, vimepungua kwa kasi katika miongo miwili iliyopita. ASN imesema mwaka 2005, haukuwa na vifo zaidi ya 1000 vinavyotokana na ndege za abiria kwa mwaka duniani kote. Taasisi ya To70 inakadiria kuwa kiwango cha ajali mbaya kwa ndege kubwa za abiria, kwa sasa ni 0.06 kwa ndege milioni moja, au ajali moja kwa kila ndege 16 milioni.
Tahadhari yatolewa kwa ajali za usafiri wa anga
Hata hivyo bado hatari ipo. Taasisi hizo mbili hazikukubaliana na hesabu ya ajali mbaya kwa mwaka 2017. Wakati taasisi ya To70 ikiripoti ajali mbili mbaya za ndege, zilizohusisha ndege ndogo, ASN, ilidai kulikuwa na ajali 10 mbaya za ndege, zilizosababisha vifo vya abiria 44 na 35 kujeruhiwa.(on the ground)
Mtandao wa ASN uliongeza kuwa hata hivyo, ajali za ndege za mizigo, zilizohuisha watu zilijumuishwa katika idadi hiyo, wakati matukio ya usafiri wa anga wa kijeshi, hayakujumuishwa.
Ilisisitizwa kuwa, hata ukizingatia matukio hayo, bado mwaka 2017, unabaki kuwa mwaka wenye idadi ndogo ya vifo vitokanavyo na ajali katika historia ya usafiri wa anga kwa sasa.
Wakati huo huo, To70 ilisisitiza kuwa, hata ajali ambazo hazikusababisha vifo bado ziliendelea kuwa tishio. Ni kutokana na matukio ya kufeli kwa injini ajali nyingine zinazohusiana na injini, ambayo sekta ya usafiri wa anga inapaswa kujiimarisha.
Kadhalika imesisitiza kuwa dosari nyingine za kiusalama zimeongezeka katika miaka ya karibuni, ikiwamo ongezeko la moto unaosababishwa na betri za lithium-ion, unaopatikana katika vifaa vya umeme kama simu za mkononi zinazobebwa katika ndege.
Kadhalika mwaka 2017, ndege ya Shirika la Ndege la Canada, Air Canada, iliponea chupuchupu kupata ajali katika tukio lililobatizwa jina la ´janga kubwa la usafiri wa anga´, baada ya ndege hiyo, almanusura kutua juu ya ndege nyingine nne, zilizokuwa katika barabara ya ndege kwenye Uwanja wa ndege wa San Francisco nchini Marekani .
Mwandishi: Florence Majani (http://www.dw.com/en/2017-the-safest-year-on-record-for-air-passengers/a-41993923)
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.