Ripoti kuhusu viwango vya ufisadi duniani yatolewa
3 Desemba 2013Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka iliyotolewa leo na Shirika la Kimataifa la kupambana na Ufisadi la Transparency International. Shirika hilo limesema kuwa kutokana na ukweli kwamba zaidi ya thuluthi mbili ya nchi zinaghubikwa na ufisadi, ni hali ambayo itaathiri ukuaji wa uchumi na kukwamisha vita dhidi ya umaskini na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa mujibu wa Shirika la Transparency International – TI lenye makao yake mjini Berlin, kuwa karibu asilimia 70 ya mataifa yote ulimwenguni yanafikiriwa kukabiliwa na “tatizo kubwa” la ufisadi katika sekta ya umma, na hakuna moja kati ya nchi 177 zilizofanyiwa utafiti mwaka huu iliyopata alama nzuri. Orodha ya kila mwaka ya TI ndicho kipimo kinachotumiwa zaidi kuangazia ufisadi katika vyama vya kisiasa, polisi, mifumo ya mahakama na utumishi wa umma, janga ambalo lina athari juu ya hatima ya maendeleo ya nchi na vita dhidi ya umaskini.
Maskini ndio wanaoumia
“Ufisadi unawaumiza sana watu maskini” amesema Mtafiti mkuu Finn Heinrich, na kuendelea kueleza kuwa hicho ndicho unachokiona wakati unapoziangalia nchi zilizoshika mkia kwenye orodha. Ndani ya nchi hizo, amesema mtafiti huyo, watu maskini ndio wanaoumia sana, na nchi hizo kamwe haitaweza kuondoka katika janga la umaskini ikiwa hazitapambana na ufisadi.
Miongoni mwa nchi ambazo zimeshuka zaidi kwenye Ripoti ya Orodha ya Ufisadi mwaka wa 2013 ni Syria inayokabiliwa na vita, pamoja na Libya na Mali, ambazo pia zimekabiliwa na migogoro ya kijeshi katika miaka ya karibuni.
Miongoni mwa nchi “zilizopiga hatua nzuri”, ijapokuwa kutoka kiwango cha chini, ni Myanmar, ambako utawala wa kijeshi umefungua milango ya mchakato wa demokrasia na huku ikineemeka na nafasi kubwa ya uwekezaji, na kugeukia zaidi sheria za uwazi na uwajibikaji. Heinrich anasema hiyo ndiyo njia pekee nchi zinaweza kuepuka “laana ya raslimali” ambako raslimali hupatikana tu kwa walio wachache na wenye uwezo. Nigeria, na nchi nyingine zenye utajiri wa mafuta bila shaka ni mifano mizuri.
Nchi zenye migogoro zinaongoza kwa rushwa
Nchi zilizoorodheshwa katika nafasi za mwisho ni pamoja na Iraq, Syria, Libya, Sudan na Sudan Kusini, Chad, Guinea ya Ikweta, Guinea Bissau, Haiti, na Yemen. Nazo nchi zilizofanya vyema ni Denmark, New Zealand, Luxembourg, Canada, Australia, Uholanzi, Uswisi, Singapore, Norway, Sweden na Dinland.
Rwanda iliyo katika nafasi ya 49 ulimwenguni imetajwa kufanya vyema katika eneo la Afrika Mashariki ikifuatwa na Tanzania iliyo katika nafasi ya 111, Kenya katika nafasi ya 136, Uganda inayokuja katika nafasi ya 140, na Burundi iliyo kwenye nafasi ya 157. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajikuta katika nafasi ya 154 kwenye orodha hiyo.
Heinrich amesema ufisadi unahusishwa na nchi zinazosambaratika kutokana na migogoro na ambazo serikali haziendeshwi kikamilifu na hivyo watu ni lazima watumie kila mbinu kuendesha harakati zao, kupata huduma, kupata chakula na kuishi.
Mtafiti huyo amesema Afghanistan ambako majeshi mengi ya magharibi yanayoongozwa NATO yanaondoka mwaka ujao baada ya kuwa nchini humo kwa zaidi ya mwongo mmoja, ni “hadithi ya kutisha”. Kwa sababu hawajaona mabadiliko yoyote makubwa. Nchi za magharibi zinawekeza kiasi kikubwa siyo tu katika masuala ya usalama lakini pia zinajaribu kurejesha mkondo wa sheria, lakini bado utafiti wa miaka ya karibuni unaonyesha kuwa idadi ya watu wanaotoa hongo bado ni ya juu kabisa ulimwenguni.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel