Ripoti: HRW yailaumu Tanzania kwa kuikuka haki za Wamaasai
31 Julai 2024Shirika la Human Rights Watchkwenye ripoti yake hiyo limebainisha matukio ya kikosi cha askari wanaosimamia hifadhi za wanyamapori wakiwashambulia na kuwapiga wakazi katika eneo hilo huku kukiwa hakuna adhabu yoyote inayochukuliwa dhidi ya maafisa hao.
Ripoti hiyo pia imesema wanajamii 13 wametoa madai ya kupigwa kati ya Septemba 2022 na Julai 2023.
Walinzi hao wa hifadhi za wanyamapori nchini Tanzania ni kama watu walio juu ya sheria imesema ripoti hiyo ambayo pia imedai kuwa serikali ya Tanzania haikuwapa watu wa jamii ya Wamaasai haki ya kujiamulia iwapo wanaridhia kuhamishwa hali ambayoHRW imesema inakiuka haki za kumiliki ardhi, kupata elimu na huduma za afya kwa wanajamii wanaohamishwa kwa nguvu.
Soma Pia: Hatua ya Tanzania kuwaondoa Wamasai yazidi kuibua hisia
Human Rights Watch imesema mvutano wa muda mrefu kati ya serikali ya Tanzania na jamii ya wafugaji ya Wamaasai wakati mwingine umesababisha vurugu mbaya, tangu serikali ilipoanzisha mpango wa kuihamisha jamii hiyo kuanzia mwaka 2022.
Takriban watu 82,000 wanatakiwa kuhamishwa kutoka eneo maarufu duniani la Hifadhi ya Ngorongoro na kupelekwa katika wilaya ya Handeni, iliyo umbali wa takriban kilomita 600 kutoka kwenye eneo lao hadi ifikapo 2027.
HRW imesema iliwahoji karibu watu 100 kati ya Agosti 2022 na Desemba 2023, wakiwemo wanajamii ambao tayari wameshahamia kwenye kijiji cha Msomera huko Handeni na wengine ambao bado wanakabiliwa na hali hiyo ya kuhamishwa.
Ripoti hiyo imesema ili kuwashinikiza watu wa eneo hilo kukubali kuondoka mamlaka ilizuia upatikanaji wa huduma muhimu kwa kupunguza ufadhili katika ujenzi wa miundombinu ya shule vituo vya afya na hivyo watu hao inawalazimu kwenda mwendo mrefu ili kupata huduma hizo.
Soma Pia: Serikali ya Tanzania imesema hakuna mapambano yoyote kati ya askari polisi na wananchi
Serikali ya Tanzania imesema hatua yake ni kwa ajili ya kulihifadhi eneo hilo dhidi ya uvamizi wa binadamu kutokana na kwamba eneo hilo ni Turathi ya Dunia lililoorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa, UNESCO. Lakini HRW imesema serikali ya Tanzania itaitumia ardhi hiyo kwa madhumuni ya kukuza utalii.
Hatua hiyo ya serikali ya Tanzania imekosolewa kimataifa huku Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya zikisimamisha ufadhili wa fedha. Benki ya Dunia ilisitisha malipo ya dola milioni 150 mnamo mwezi Aprili fedha ambazo zingelitumiwa kuhifadhi mbuga na Umoja wa Ulaya pia umebatilisha ustahiki wa Tanzania wa kupokea ufadhili wa dola milioni 19 kwa ajili hiyohiyo ya kuhifadhi mbuga.
HRW imesema imegundua kwamba serikali inawanyamazisha wakosoaji hali inayochangia pakubwa watu kuwa na hofu. Imemnukuu mtu mmoja ambaye tayari ameshahamia katika kijiji kipya cha Msomera akisema "Mtu hawezi kusema lolote.”
Chanzo:AFP