1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa hatashitakiwa kwa kashfa ya "farmgate"

11 Oktoba 2024

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini hatakabiliwa na mashitaka kwenye kashfa ya fedha taslimu zilizofichwa kwenye nyumba yake iliyoibuliwa miaka miwili iliyopita na kupelekea uchunguzi maalum wa polisi.

https://p.dw.com/p/4lenm
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.Picha: Kim Ludbrook/Pool EPA/dpa/picture alliance

Waendesha mashitaka walisema hapo jana kwamba uamuzi wa kutomshitaki Ramaphosa au mwengine yeyote kwenye kadhia hiyo umechukuliwa baada ya uchunguzi wa kina.

Kashfa hiyo iliyopewa jina la "farmgate" ilihusisha tuhuma za kuibiwa kwa dola 580,000 taslimu kwenye nyumba ya shambani ya rais huyo wa Afrika Kusini, wizi uliokuja kubainika na mmojawapo wa walinzi wake.

Soma zaidi: Ramaphosa akabiliwa tena na mchakato wa kumuondowa

Inatajwa kuwa Ramaphosa alikuwa ameficha kiwango hicho kikubwa cha fedha kwenye kochi ili kukwepa mamlaka za ukaguzi wa fedha za kigeni.

Upinzani ulitumia hoja hiyo kulitaka bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani naye mwishoni mwa mwaka 2022, lakini chama chake, ANC, kilitumia wingi wake bungeni kuzuwia mchakato huo.