1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Pakistan, Pervez Musharraf ahukumiwa kifo

Babu Abdalla17 Desemba 2019

Mkuu wa majeshi wa zamani wa Pakistan ambaye pia alikuwa rais wa nchi hiyo Pervez Musharraf amehukumiwa kifo na mahakama ya kupambana na ugaidi nchini humo baada ya kukutikana na hatia ya uhaini.

https://p.dw.com/p/3UwpN
Pakistan Ex-Präsident Pervez Musharraf
Picha: Getty Images/AFP/A. Qureshi

Mahakama ya kupambana na ugaidi nchini Pakistan imemuhukumu kifo aliyekuwa mtawala wa kijeshi nchini humo Pervez Musharraf kwa kosa la  uhaini na kuizuia katiba. Jopo la majaji watatu lilitangaza hukumu hiyo katika mji mkuu wa Islamabad baada ya miaka kadhaa ya kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani. 

Musharraf ambaye aliiongoza Pakistan kati ya mwaka 1999 na 2008 sasa si mtuhumiwa tena bali ni mfungwa.

Hii ni mara ya kwanza kwa mahakama za Pakistan kutoa hukumu ya aina hiyo dhidi ya kiongozi wa zamani ambao mara nyingi wamekuwa wakionekana kuwa juu ya sheria na kupata kinga dhidi ya kushtakiwa.

"Ni uamuzi wa kihistoria ambao utafungua upya historia ya siasa" alisema Hamid Mir ambaye ni mtangazaji katika runinga moja nchini humo.

Mtawala huyo wa zamani wa kijeshi ambaye sasa anaishi uhamishoni Dubai, alimuondowa madarakani aliyekuwa waziri mkuu Nawaz Shariff katika mapinduzi ya kijeshi bila umwagikaji wa damu mnamo mwaka 1999.

Musharraf alipata umaarufu duniani baada ya kujiunga na vita dhidi ya ugaidi vilivyoongozwa na Marekani nchini Afghanistan.

Pia aliisitisha katiba ya mwaka 2007 kinyume cha sheria ili asalie mamlakani.

Baada ya hukumu hiyo, Musharraf hakupatikana ili kutoa maoni yake kutokana na hukumu hiyo dhidi yake.

Rais wa zamani wa Pakistan Jenerali Pervez Musharraf. (Picha ya maktaba)
Rais wa zamani wa Pakistan Jenerali Pervez Musharraf. (Picha ya maktaba)Picha: picture-alliance/dpa

Amekuwa akiishi Dubai katika falme za kiarabu na anasemekana kuwa mgonjwa sana, na hivyo basi kunafanya uwezekano wake kurudi Pakistan kuwa mgumu.

Hoja nyengine ambayo pia inafanya hukumu dhidi yake kuwa katika mashaka ni kutokuwepo makubaliano kati ya Pakistan na Dubai ya kumrudisha Musharraf nchini mwake ili kukabiliwa na hukumu hiyo. Iwapo angeweza kurudi Pakistan, kisheria ana uwezo wa kuipinga hukumu hiyo mahakamani.

Katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video, Musharraf ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali moja Dubai alisema kuwa yuko tayari kutoa taarifa yake kuhusu kesi inayomkabili ya uhaini lakini hawezi kusafiri Pakistan.

Baada ya hukumu hiyo kutangazwa, waziri wa habari wa Pakistan Firdous Ashiq Awan aliwambia waandishi wa habari kuwa waziri mkuu Imran Khan atatoa tamko lake baadaye kuhusu hukumu iliyotolewa  baada ya kuisoma kwa kina hukumu hiyo.

Wakuu wa majeshi wameiongoza nchi hiyo kwa muda mrefu tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1947.

Vyanzo: Reuters/AP/DPA