1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter afariki

30 Desemba 2024

Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100. Carter alihudumu katika Ikulu ya White House kuanzia mwaka wa 1977 hadi 1981. Alifariki akiwa nyumbani kwake Plains.

https://p.dw.com/p/4ofjO
Rais wa zamani Jimmy Carter akijibu maswali ya waandishi habari katika Kituo cha Carter, mjini Atlanta Georgia, Agosti 20, 2015
Jimmy Carter alikuwa rais wa 39 wa MarekaniPicha: John Amis/REUTERS

Taasisi yake ya Kituo cha Carter imesema rais huyo wa zamani alifariki akiwa nyumbani kwake mjini Plains, akiwa amezungukwa na familia yake.

"Baba yangu alikuwa shujaa, sio kwangu tu lakini kwa kila mmoja anayeamini katika amani, haki za binaadamu, na upendo usio na ubinafsi,” amesema mwanawe wa kiume, Chip Carter.

"Ulimwengu ni familia yetu kwa sababu ya jinsi alivyowaleta watu pamoja, na tunakushukuru kwa kuheshimu kumbukumbu yake kwa kuendelea kufuata imani hizi za pamoja.”

Rais wa kwanza wa Marekani kufikisha miaka 100

Mdemocrat Carter, rais wa 39 wa Marekani, aliishi muda mrefu zaidi baada ya muhula wake madarakani kuliko rais mwingine yeyote wa nchi hiyo.

Muhula wake unakumbukwa hasa kwa matukio ya kihistoria katika Mashariki ya Kati. Ni pamoja na kusimamia mikataba ya Amani ya Camp Dave ya mwaka wa 1978 kati ya Misri na Israel. Hii ilipelekea kupatikana mkataba wa kihistoria wa amani kati ya nchi hizo mbili katika mwaka wa 1979. Pia alikuwa rais wakati Marekani ilipofanikisha mazungumzo ya kuwachiwa huru wafanyakazi 52 waliokuwa wamezuiliwa kwenye ubalozi wa Marekani mjini Tehran.

Jimmy Carter, rais wa 39 wa Marekani afariki dunia akiwa na umri wa miaka 100
Carter alikuwa na nafasi muhimu katika kikundi cha Wazee kilichoanzishwa na Nelson MandelaPicha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Walichukuliwa mateka baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka wa 1979 kwa siku 444. Baada ya kushindwa kupata muhula wa pili madarakani, Carter akaanzisha Kituo cha Carter. Mateka hao waliachiwa dakika chache baada ya kuapishwa kwa Ronald Reagan mwaka wa 1981.

Alilenga kuongoza juhudi za amani kimataifa, kutetea demokrasia, afya ya umma na haki za binadamu.

Carter alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kuzaliwa katika hospitali, Oktoba 1, 1924 mjini Plains, jimboni Georgia. Mama yake alikuwa muuguzi na mmiliki wa duka la jumla. Baada ya maisha ya utotoni yaliyogubikwa na kipindi cha Mtikisiko Mkubwa kiuchumi, alijiunga na Chuo cha Jeshi la Wanamaji na akapendana na rafiki wa dada yake Rosalynn Smith. Walioana mwaka wa 1946 na wakaishi Pamoja kwa miaka 77, hadi Rosalynn alipofariki Novemba 2023 akiwa na umri wa miaka 96.

Viongozi watuma salamu za rambirambi

Rais anayeondoka Joe Biden amewaongoza marais wa Marekani na viongozi wengine wa dunia kutuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Carter. "Marekani na ulimwengu imempoteza kiongozi wa ajabu, mzee wa taifa na mfadhili wa kibinaadamu,” Alisema Biden katika taarifa iliyotolewa na White House. Kisha aliongeza baadae katika hotuba ya televisheni kuwa Carter "aliishi maisha yaliyopimwa sio kwa maneno bali kwa matendo yake.”

Rais Joe Biden wa Marekani
Rais Joe Biden amesema amempoteza rafiki mpendwaPicha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Rais mteule Donald Trump alisema Wamarekani wanapaswa kumlipa Carter "deni la shukrani." "Changamoto ambazo Jimmy alikabiliana nazo akiwa rais zilikuja katika wakati muhimu kwa nchi yetu na alifanya kila awezalo kuboresha maisha ya Wamarekani wote," alisema kwenye mtandao wa kijamii.

Miongoni mwa marais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton alisema mtangulizi wake "alifanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya ulimwengu ulio bora na wa haki."

George W. Bush alisema Carter "aliiheshimu ofisi. Na juhudi zake za kuwa na ulimwengu bora hazikuishia na urais."

Barack Obama alimsifu Carter kwa kutufundisha "sote maana ya kuishi maisha ya neema, heshima, haki na huduma."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Carter atakumbukwa "kwa mshikamano wake na walio hatarini, neema yake ya kudumu, na imani yake isiyo na kikomo katika manufaa ya wote na ubinadamu wetu wa pamoja."

Afp, reuters, ap, dpa