Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor aanza kujitetea.
14 Julai 2009Rais wa Zamani wa Liberia, Charles Taylor, leo hii amepanda katika kizimba cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya mjini The Hague, uholanzi, na kukana mashitaka yanayomkabili, likiwemo la uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kupata fursa ya kujitetea katika mahakama hiyo tangu kufunguliwa mashitaka hayo yanayodaiwa kufanyika wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1991 na 2001.
Mbabe huyu wa kivita alisema tuhuma hizo anazohusishwa nazo, zikiwemo za mauaji na ubakaji, ni uongo na uzushi mtupu ambazo zinatokana na kutokuwepo kwa taarifa sahihi.
Akifafanua zaidi pale alipotakiwa kufanya hivyo na wakili wake wa Utetezi, Taylor amesema ni jambo lisilowezekana yeye kushiriki katika uhalifu wa namna hiyo.
Aidha mtuhumiwa huyu, mwenye umri wa miaka 61, ameongeza kuwa si miongoni mwa wahalifu, hajawahi na hatokuwa hata kama watafikiri hivyo au sivyo.
Taylor ni Kiongozi wa kwanza Barani Afrika kupandishwa kizimbani katika mahakama ya uhalifu wa kivita kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Hata hivyo, anatarajiwa kuwasilisha utetezi wake unaonesha kuwa alikuwa akistawisha amani zaidi ya kuchochea vita katika maeneo ya Afrika Magharibi.
Wakili wa Charles Taylor, aliyoongoza upande wa utetezi, Courtenay Griffths, alikanusha kuwa kiongozi huyo alikuwa mkatili kiasi cha kuitwa Napoleone wa Afrika.
" Tunafikiri hapa mahakama ya kimataifa ni eneo la mstari wa mbele la haki la kimataifa, nadhani ni sehemu muhimu ambayo kila mtuhumiwa ataweza kupata haki inayostahili. Na katika mashitaka haya, tunasema kwamba bwana Taylor hana hatia, na tupo hapa kulinda maslahi yake na kuonesha ukweli."
Hii ni mara ya kwanza kusimama kizimbani tangu kuanza kwa mashitaka yake miezi 18 iliyopita.
Taylor, aliyekuwa amevaa suti ya rangi ya kiijvu cheusi, huku akiwa na shati jeupe na tai yenye vitone, alitoa utetezi wake kwa umakini mkubwa.
Kabla hajasema lolote alikohoa kidogo ili kusafisha koo lake, kisha akamwambia Jaji."Jina langu Dakpenah Charles Ghankay Taylor, rais wa 21 wa Jamhuri ya Liberia."
Aliendelea: "Nimetumia sehemu kubwa ya maisha yangu kufanya nilichodhani kuwa ni haki",aliongoza kiongozi huyo wa zamani wa Liberia.
Kiongozi huyo amepandishwa kizimbani kujibu tuhuma 11 zinazomkabili zikiwemo za mauaji, ubakaji na kuwaandikisha watoto wadogo jeshini.
Zaidi ya watu laki moja walipoteza maisha katika mgogoro huo wa 1991 hadi 2001.
Charles Taylor alikuwa rais wa Liberia mwaka 1997 na baadae aliondolewa madarakani na kwenda kuishi uhamishoni mwaka 2003.
Mbabe huyo wa Kivita alifikishwa katika mahaka maalum nchini Sierra Leone baada ya kukamatwa nchini Nigeria na baadae kusafirshwa mpaka The Hague Uholanzi.
Mwandishi-Sudi Mnette AFPE
Mhariri -Othman Miraji.