1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Zelensky asema hali ni mbaya Donetsk

Josephat Charo
8 Oktoba 2024

Jeshi la Ukraine linasema limezitungua droni 18 za Urusi usiku wa kuamkia leo, huku wizara ya ulinzi ya Urusi ikitangaza kuudhibiti mji wa Zota Nyva mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4lXDq
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine
Rais Volodymyr Zelensky wa UkrainePicha: president.gov.ua/en

Urusi ilitumia makombora mawili ya masafa marefu aina ya Iskander-M na droni 19 katika shambulizi la usiku, lakini jeshi la anga la Ukraine likaziangusha droni 18 na ya 19 ikarudi katika himaya ya Urusi.

Jeshi la anga la Ukraine limesema vikosi vya Urusi vimetumia droni na makombora katika shambulizi kwenye eneo la kusini la Ukraine la Odesa. Gavana wa Odesa Oleh Kiper amesema shambulizi hilo la droni katika mji wa Chormomorsk limesababisha moto katika ghorofa tatu za jengo la makazi ya watu lakini halikusababisha vifo wala majeruhi.

Gavana huyo aidha amesema shambulizi hilo pia limesababisha moto katika jengo la afisi za utawala na utengenezaji bidhaa katika wilaya ya Odesa, wakati droni hiyo ilipoanguka katika eneo la wazi bila kulipuka.

Soma pia: Zelensky aomba msaada washirika wake

Kombora la Urusi pia limekipiga chombo chenye bendera ya Palau katika bandari ya Odesa na kumuua raia mmoja wa Ukraine na kuwajeruhi wafanyakazi watano wa chombo hicho cha majini, katika shambulizi la pili la aina hiyo kuwahi kufanywa katika kipindi cha siku nyingi za utulivu.

Shambulizi la Urusi katika mji wa kaskazini mashariki wa Kharkiv nchini Ukraine limewajeruhi watu 11, akiwamo mtoto mmoja. Gavana wa eneo hilo Oleh Syniehubov amesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba shambulizi hilo limeharibu miundombinu na maafisa walikuwa wakihakiki aina ya silaha zilizotumiwa.

Hali inalezwa kuwa mbaya katika mji wa Donetsk
Hali inalezwa kuwa mbaya katika mji wa DonetskPicha: Ukraine National Police via AP/picture alliance

Akizungumza usiku wa kuamkia, rais wa Ukraine Volodymry Zelensky amesema hali katika eneo la Donetsk inabaki kuwa ya changamoto. Amesema watajaribu kuwashawishi washirika wao katika mkutano ujao huko Ramstein Ujerumani kuhusu haja ya dharura ya kuimarisha uwezo wao na maeneo yao sasa hivi, wakati wa miezi hii ya msimu wa mapukutiko.

"Tunawaalika washirika wetu watoe muelekeo kuhusu wanavyopanga kuvifikisha mwisho vita hivi, nafasi ya Ukraine katika muundo wa ulinzi wa dunia na hatu aza pamoja zinaweza kuvielekeza vita hivi kufika mwisho. Kufikia mwisho wa siku hivi leo, natarajia ripoti kutoka kwa timu yetu ambayo wa sasa inafanya kazi mjini Washington, kufuatia kuanza kwa kazi ya kuainisha vipngele vya hatua za kijeshi na kisiasa za mpango wa ushindi"

Matumaini ya mkutano wa Ramstein

Kamanda wa majeshi ya Ukraine Oleksandr Syrskyi, alisema kwamba amejadili kipengele cha kijeshi cha mpango wa ushindi wa vita wa Ukraine wakati wa mazungumzo ya simu na Jenerali wa jeshi la Marekani C.Q. Brown. Syrskyi pia amesema amemuelezea Brown kuhusu hali ilivyo katika uwanja wa vita na mahitaji muhimu ya dharura ya Ukraine kabla mkutano wa Ramstein Oktoba 12.

Ukraine ingali inasubiri kauli kutoka kwa washirika wake wa kambi ya Magharibi kuhusu maombi yake ya mara kwa mara kutumia silaha za masafa marefu kuyalenga maeneo yaliyo katika ardhi ya Urusi. Maendeleo kuhusu suala hilo huenda yakapatikana wikendi ijayo katika mkutano utakaofanyika kambi ya jeshi la Marekani mjini Ramstein Ujerumani, wakati viongozi wa idara za ulinzi kutoka nchi washirika zaidi ya 50 wanaoratibu msaada ya kijeshi kwa Ukraine wanatarajiwa kukutana.

Wakati haya yakiarifiwa, jeshi la Urusi limesonga mbele kuingia eneo la mashariki la mji unaozozaniwa wa Toretsk nchini Ukraine. Msemaji wa jeshi la Ukraine, Anastasia Bobovnikova, amesema mapigano yanaendelea Toresk kwenyewe na hali si shwari. Amesema mapiganao ni ya nyumba kwa nyumba.

(afp, reuters)