1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya Muungano wa Korea

14 Oktoba 2015

Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck akiwa ziarani Korea ya kusini,amelitembelea eneo marufuku kwa silaha linalozigawa Korea mbili na kuhudhuria maonyesho ya matumaini ya kuungana upya Korea mbili.

https://p.dw.com/p/1GndU
Rais Gauck akitembelea eneo la mpaka unaoigawa KoreaPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Akiendelea na ziara yake iliyoanza jumapili iliyopita,rais Joachim Gauck amelitembelea hii leo eneo la mpakani,miaka 70 baada ya Korea mbili kugawika.Katika eneo hilo linalojulikana kama Panmunjom,rais Gauck alifuatana na mkuu wa tume isiyoelemea upande wowote ya kimataifa inayosimamia makubaliano ya kuweka chini silaha,meja jenerali Urs Gerber wa Uswisi.Katika eneo hilo mpaka leo bado malaki ya wanajeshi wa nchi hii iliyogawika wanakodoleana macho.

Mwezi uliopita wa Agosti tu wanajeshi wawili wa Korea ya kusini walijeruhiwa vibaya sana mzizinga iliyozikwa ardhini iliporipuka.

Katika eneo hilo la Panmunjom ndiko yalikotiwa saini mwaka 1953 makubaliano ya kuweka chini silaha kati ya Korea mbili.Makubaliano ya amani mpaka leo bado hayajafikiwa.

Matumaini ya kuungana upya Korea yapaliliwa

Kabla ya hapo rais wa shirikisho Joachim Gauck akifuatana na waziri wa muungano Hong Yong pyo na viongozi wengine wa serikali, alitembelea maonyesho ya muungano katika kituo cha safari za reli cha Dorosdan-kituo cha mwisho cha reli inayotokea mji mkuu Seoul.Katika maonyesho hayo yanaonyesha picha za jinsi Ujerumani ilivyokuwa imegawika na pia kuhusu kugawika Korea.Miongoni mwa picha hizo inakutikana ile ya ukuta wa Berlin na behewa la treni iliyokuwa ikisafiri katika eneo la mpaka uliokuwa ukiigawa Ujerumani.

Südkorea Joachim Gauck erhält die Ehrenbürgerurkunde der Stadt Seoul
Rais Gauck ametunukiwa shahada ya mkaazi wa heshima wa jiji la SeoulPicha: picture-alliance/dpa/J. Heon-Kyun

Akihutubia katika maonyesho hayo rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani amesifu moyo na matumaini ya wakorea ya kusini katika kuona nchi yao inaungana upya .

"Kwa umakini na hima unawapa wanasiasa,wake kwa waume wa nchi hii,moyo na matumaini.Tunabidi tutambue hatujui lini matumaini haya makubwa ya wakorea ya kuungana upya yatakamilika.Lakini kimoja tunakijua vilivyo,hakuna kitakachotekelezeka bila ya moyo huu wa matumaini."Amesema rais Gauck.

Ushirikiano wa pande mbili kuimarishwa

Watu kama 300 hivi walishiriki pia katika sherehe hizo.

Südkorea Joachim Gauck und Park Geun-Hye
Rais Gauck na mwenyeji wake rais Park Geun-HyePicha: Reuters/J. Heon-Kyun

Jana rais Joachiom Gauck alikuwa na mazungumzo pamoja na rais Park Geun hye na kuahidi kushirikiana katika juhudi za kuigeuza Korea ya kaskazini iwe nchi iliyotakasika na silaha za kinuklea pamoja na kuimarisha hali ya haki za binaadam Korea kaskazini.Rais Geun alishauri uungaji mkono wa Ujerumani katika kuziunganisha upya Korea mbili akisema hali ya kuamainiana na mchango wa usalama kutoka nchi jirani zilikuwa muhimu zaidi katika kurahisisisha kuungana upya Ujerumani.

Rais Joachim Gauck anapanga kuondoka Seoul leo kuelekea Mongolia.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Agenturvideos/Dopesheets

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman