1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Timor Mashariki pamoja na waziri mkuu waponea chupuchupu majaribio ya kutaka kuwaua

11 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D5g2

Rais wa Timor Mashariki, Jose Ramos-Horta, pamoja na waziri wake mkuu, Xanana Gusmao, wameponea chupuchupu majaribio ya kutaka kuwaua.

Rais Ramos Horta amepigwa risasi tumboni katika shambulio lililofanywa alfajiri ya leo nyumbani kwake nje ya mji mkuu Dili.

Kiongozi huyo amepelekwa nchini Australia kwa matibabu ya dharura.

Duru zinasema maisha ya rais Ramos Horta hayamo hatarini licha ya majeraha aliyoyapata na kwamba kiongozi huyo anasaidiwa kupumua kutumia kifaa maalum.

Msemaji mmoja wa serikali ya Timor Mashariki amesema shambulio dhidi ya rais lilipangwa.

Rais Horta alifanyiwa upasuaji mjini Dili kabla kusafirishwa katika mji wa kaskzini wa Austarlia Darwin kwa upasuaji zaidi.

Mmoja kati ya walinzi wa rais Ramos Horta na mshambuliaji mmoja wameuwawa katika mapambano ya risasi yaliyotokea wakati watu waliokuwa wamejihami na bunduki walipoifyatulia risasi nyumba ya rais katika kitongoji cha mji mkuu Dili.

Mshambuliaji aliyeuwawa ametambuliwa kuwa Alfredo Reinado, kiongozi wa waasi aliyekuwa akitafutwa kwa mashtaka ya mauaji.

Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulio la pili lililomlenga waziri mkuu wa Timor Mashariki, Xanana Gusmao.

Maafisa wanasema hali mjini Dili imedhibitiwa.