1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Tanzania awaapisha viongozi walioteuliwa

Salma Said1 Septemba 2023

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaapisha siku ya Ijumaa viongozi aliowateua siku kadhaa zilizopita katika mabadiliko mengine makubwa ya Baraza lake la Mawaziri yaliyoshuhudia nafasi mpya ya Naibu Waziri Mkuu.

https://p.dw.com/p/4Vq48
Tansania Sansibar Präsidentin Samia Suluhu Hassan bei Kizimkazi Festival
Picha: Presidential Press Service Tanzania

Halfa ya kuapishwa viongozi hao wateule imefanywa Ikulu ndogo ya Zanzibar. Kwenye hotuba yake rais Samia amesema mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha ufanisi wa kazi serikalini.

Baada ya shughuli ya kuapisha ambayo pia ilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi, Rais Samia katika Hotuba yake fupi amesisitiza swala la uwajibikaji na mabadiliko yatakayoleta tija katika serikali na kwa wananchi.

Soma pia: Rais Samia afanya mabadiliko ya baraza la mawaziri

Rais Mwinyi alipewa nafasi ya kuzungumza katika hafla hiyo ambapo aliwashajiisha mawaziri juu ya kuendeleza ushirikiano kati ya Zanzibar na wizara za Muungano ili kuimarisha zaidi Muungano na kusema kwamba anaridhishwa na maridhiano yanayooneshwa kati ya pande hizo mbili hizo za muungano.

Tansania Sansibar Präsidentin Samia Suluhu Hassan bei Kizimkazi Festival
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali katika sherehe za Kizimkazi visiwani Zanzibar Agosti 2023Picha: Presidential Press Service Tanzania

Miongoni mwa walioapishwa ni Dotto Biteko ambaye anakuwa Naibu Waziri Mkuu, nafasi mpya iliyoundwa kusaidia uratibu shughuli za serikali. Nafasi hiyo isiyo ya kikatiba iliwahi kuwepo mwanzoni mwa miaka ya 1990 enzi ya utawala wa rais Ali Hassan Mwinyi. Biteko pia ataongoza Wizara ya Nishati na Madini.

Viongozi wa Zanzibar wahudhuria pia hafla hiyo

Waliohudhuria hafla hiyo ni karibu viongozi wote wajuu wa serikali ya Muungano na Zanzibar wakiongozwa na Makamu wa Rais Philip Mpango ambaye aliwataka mawaziri kutekeleza majukumu yao vyema ili serikali ya CCM iendelele kuaminiwa hasa wakati wa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Soma pia:Rais Samia ahitimisha tamasha la Kizimkazi Zanzibar 

Hafla ya kuwaapisha mawaziri hao walioteuliwa hivi juzi ilihudhuriwa na pia na Makamo wa kwanza wa Rais na mawaziri mbali mbali pamoja na viongozi wengine.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwaapisha mawaziri visiwani Zanzibar.