Katika mabadiliko hayo yaliyoshtua wengi, Rais Samia amemuondosha Katibu Mkuu Kiongozi, Hussein Omary Kitanga na kumpeleka kuwa balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mjini New York, wakati aliyekuwa akishika wadhifa huo, Balozi Profesa Kennedy Gaston amefutwa kazi.
Rais Samia pia amemteua aliyekuwa katibu mkuu ikulu, Moses Kusiluka kuwa katibu mkuu kiongozi ilihali aliyekuwa mkuu wa idara ya usalama wa taifa, Kamishna Diwani Athmani Msuya akiteuliwa kuwa katibu mkuu ikulu.
Nafasi ya Kamishna Diwani Msuya sasa imechukuliwa na Said Hussein Masoro aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi wa shughuli za ndani wa Usalama wa Taifa.
Katika hotuba yake fupi kwa taifa kuhusiana na mabadiliko hayo, Rais Samia amesema ameamua kutupia macho eneo la ubalozi kutokana na ukweli kwamba baadhi ya ofisi hizo zimekuwa na rekodi isiyoridhisha kwa matumizi mabaya ya fedha na madaraka.
Mabadiliko yazua gumzo miongoni mwa wachambuzi
Mabadiliko hayo yamekuwa yakichambuliwa na wengi kama ishara ya Rais Samia kuanza kujipanga upya na kujiimarisha wakati akijiandaa kukumilisha kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano mwaka 2025.
Mchambuzi Bernard Eric anasema kile kinachochukuliwa na Rais Samia ni hatua inayoweza kuchukuliwa na kiongozi yoyote wa nchi pale anapoona kuwepo haja ya kupanga upya safu yake ili kuimarisha utendaji wa serikali.
Taarifa ya ikulu imesema kuwa mabadiliko hayo yanaanza mara moja. Kumekuwa na fununu juu ya Rais Samia kuifanyia mabadilko makubwa safu yake ya uongizi na hali hiyo inadhihirisha na ukweli wa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni wakati alipokuwa akihitimisha mkutano mkuu wa chama chake CCM.
Alisisitiza kuwa yuko mbioni kuipanga upya serikali yake ingawa hakudokeza ni maeneo gani yatakumbwa na pangua pangua hiyo.