Biden aihakikishia Ufilipino ushirika madhubuti wa kiulinzi
2 Mei 2023Rais wa Marekani Joe Biden amemwambia mwenzake wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr kwamba Marekani itaendelea kuwa mshirika wake madhubuti wa kiulinzi ikiwemo katika eneo la Kusini mwa bahari ya China ambako nchi hiyo ya Ufilipino inakabiliwa na shinikizo kutoka China.
Rais Marcos Jr. ambaye ziara yake katika Ikulu ya Marekani, ni ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa juu katika kipindi cha miaka 10 wa Ufilipino amesisitiza juu ya umuhimu wa Marekani kama mshirika pekee wa nchi yake katika mkataba wa kiulinzi kwenye eneo hilo kutokana na kile alichosema hali tete ya siasa za kieneo zinazoshuhudiwa wakati huu.
Maafisa wa Marekani wamesema viongozi hao wawili wataingia kwenye makubaliano ya miongozo mipya katika ushirikiano imara zaidi wa kijeshi, pamoja na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi.
Serikali mjini Washington inaitazama Ufilipino kama nchi muhimu katika juhudi zozote za kuukabili uvamizi wa China wa Kisiwa cha Taiwan chenye mamlaka yake ya ndani ambacho China inadai kukimiliki.