Rais wa Mamlaka ya Palestina Abbas azuru mji wa Jenin
12 Julai 2023Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas leo ameitembela kambi ya wakimbizi ya mji wa Jenin iliyopo eneo la Ukingo wa Magharibi kiasi wiki moja tangu vikosi vya Israel vilipouvamia mji huo kwa operesheni ya kijeshi iliyosababisha vifo vya Wapalestina 12.
Soma pia: Vifo vyaongezka operesheni ya kijeshi ya Israel mjini Jenin
Abbas ameitaja kambi hiyo kuwa "alama ya mapambano" na kuahidi kuijenga upya pamoja na mji wa Jenin ambavyo kwa sehemu kubwa vimeharibiwa na uvamizi wa vikosi vya Israel. Abbas amesema ziara yake imelenga kuonesha kuwa Palestina ni moja iliyo chini ya serikali moja na kuwaonya wote wanaojaribu kuhujumu mshikamano na usalama wa Wapalestina.
Hiyo ilikuwa ziara ya kwanza ya kiongozi huyo kwenye kambi hiyo katika kipindi cha karibu miongo miwili iliyopita. Imefanyika wakati idadi kubwa ya Wapalestina wanaonesha kuvunjwa moyo na utawala Abbas kutokana na mashaka kubwa umepoteza udhibiti wa eneo hilo linalotajwa kuwa ngome ya makundi ya wanamgambo.