1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Madagascar ateuwa waziri mkuu mpya

4 Juni 2018

Rais wa Madagascar amemteuwa afisa wa juu wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu, kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa, katika juhudi za kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.

https://p.dw.com/p/2yvAy
Amtseinführung Madagaskar Hery Rajaonarimampianina
Rias wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina.Picha: picture alliance/ZUMA Press

Rais Hery Rajaonarimampianina ameteua Christian Ntsay, ambaye kwa sasa anafanya kazi katika shirika la kazi duniani ILO kushika wadhifa huo, baada ya waziri mkuu aliekuwepo Olivier Solonandrasana kujiuzulu mapema Jumatatu.

Taifa hilo la kisiwa lililoko katika bahari ya Hindi limetikiswa na maandamano yaliyonuwia awali kupinga sheria mpya za uchaguzi ambazo upande wa upinzani ulisema zilibuniwa ili kuwazuwia wagombea wao kushiriki uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

Mahakama ya katiba imemuamuru Rais Hery Rajaonarimampianina kuunda serikali ya umoja wa kitaifa yenye waziri mkuu anayekubalika na pande zote ili kuepusha mgogoro mkubwa zaidi. Na hilo kufanyika, serikali ya sasa ilitakuwa kujizulu na rais aliamriwa kumteuwa waziri mkuu mpya ifikapo Juni 12.

Ntsay mwenye 57, siyo mwanachama wa chama chochote cha siasa, na ana sifa ya kuwa mtaalamu wa kimataifa katika usimamizi wa mausala ya ajira na uongozi, na aliwahi kuwa waziri wa utalii wa Madagascar kati ya 2002 na 2003.

Madagascar Premierminister Olivier Solonandrasana Mahafaly
Waziri Mkuu aliejiuzulu Olivier Solonandrasana.Picha: picture-alliance/AP Images/F. Mori

Waziri mkuu wa zamani Olivier Mahafaly Solonandrasana alitangaza kujiuzulu mbele ya vyombo vya habari mapema leo, ili kuepusha kuwa "kizingiti katika maisha ya mataifa hilo."

Vuguvugu la kumuondoa Rajaonarimampianina

Tangu Aprili 21 wafuasi wa vyama vya upinzani wameukalia uwanja wa Mei 13 mjini Antananarivo, awali kupinga mapendekezo ya rais ya kuufanyia mabadiliko mfumo wa uchaguzi. Lakini baada ya mapendekezo hayo kutupiliwa mbali na mahakama, maandamano hayo yaligeuka vuguvugu kubwa la kumuondoa madarakani Rajaonarimampianina.

Rais huyo alijitokeza kwenye mkutano wa waandishi habari sambamba na waziri mkuu wake wa zamani siku ya Jumatatu, na kuthibitisha kuwa ingawa serikali imejiuzulu, itabakisha mamlaka yake katika kipindi cha mpito. Alisema wakati wanasubiri kutangaza serikali mpya, Solonandrasana na timu yake wataendelea kuwepo kushughulikia masuala ya sasa.

Mahakama ya Katiba iliamuru kwamba muundo wa serikali mpya unapaswa kuakisi kwa usawa matokeo ya uchaguzi uliopita wa bunge mwaka 2013. Lakini hukumu hiyo imesababisha mjadala mkali kati ya serikali na upinzani kuhusiana na tafsiri yake.

Wahlen Madagaskar Andry Rajoelina
Rais wa zamani wa Madagascar Andry Rajoelina.Picha: picture alliance/ landov

Malumbano kuhusu tafsiri ya hukmu ya mahakama

Pande zote mbli zinasema ndiyo zina wingi mkubwa bungeni, ambako wabunge wamekuwa wakibadilisha vyama tangu 2013. Mwishoni mwa wiki, Rajaonarimampianina alikataa majina matatu ya waziri mkuu wa maridhiano yalioywasilishwa kwake na upinzani, ambao wanatoka katika chama cha Mapar kinachoongozwa na rais wa zamani Andry Rajoelina.

Juhudi za ndani na za kimataifa kuutatua mgogoro katika taifa hilo ambalo ni koloni la zamani la Ufaransa zimeshindwa kufua dafu. Juhudi za karibuni zaidi, ambazo ni mkutano wa baraza la maridhiano la kitaifa uliohusisha wajumbe wa serikali na upinzani, ulimalizika bila muafaka siku ya Ijumaa.

Waziri wa ulinzi Beni Xavier Rasolofonirina alitishia kutumia vikosi vya usalama ikiwa juhudi za kisiasa zitashindwa kutatua mgogoro huo wa kisiasa.

Mwandisi: Iddi Ssessanga/afpe,adpe,rtre

Mhariri: Josephat Charo