George Weah akubali kushindwa katika uchaguzi wa rais
18 Novemba 2023Akilihutubia taifa kwa njia ya redio Ijumaa jioni, Weah alisema kuwa ingawa matokeo yaliyotolewa hadi wakati huo hayakuwa ya mwisho yanaashiria kuwa Bokai anaongoza kwa kiasi ambacho hawezi tena kumpiku.
Maafisa wa uchaguzi wanasema wakati asilimia 99.58 ya kura zikiwa zimehesabiwa, Boakai alikuwa anaongoza kwa asilimia 50.89 dhidi ya asilimia 49.11% alizopata Weah. Matokeo hayo yalikuwa kinyume na matokeo ya uchaguzi wa miaka sita iliyopita, wakati Weah alipomshinda Boakai kwa urahisi katika duru ya pili.
Weah awataka wafuasi wake kukubali matokeo ya uchaguzi huo
Kiongozi huyo amewahimiza wafuasi wake kuiga mfano wake na kukubali matokeo ya uchaguzi huo akiongeza kuwa wakati wao utakuja tena mwaka 2029.
Hotuba hiyo ya Weah, imetolewa hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa nchini humo wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la wasiwasi kuhusu kuzorota kwa demokrasia katika mataifa ya Afrika Magharibi.