1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Yoon akabiliwa na jaribio jipya la kukamatwa

8 Januari 2025

Rais wa Korea Kusini aliyesimamishwa kazi Yoon Suk Yeol anakabiliwa na jaribio jipya la kukamatwa baada ya mkuu wa timu ya uchunguzi kuapa kwamba watafanya kila liwezekanalo kuvunja vizuizi vyote vya ulinzi.

https://p.dw.com/p/4ow85
Korea Kusini | Yoon Suk Yeol | Seoul
Rais wa Korea Kusini aliyesimamishwa kazi na bunge Yoon Suk YeolPicha: South Korean Presidential Office/Handout/Yonhap/AFP

Rais wa Korea Kusini aliyesimamishwa kazi Yoon Suk Yeol anakabiliwa na jaribio jipya la kukamatwa baada ya mkuu wa timu ya uchunguzi kuapa kwamba watafanya kila liwezekanalo kuvunja vizuizi vyote vya ulinzi na kiusalama na kumchukua kiongozi huyo aliyefunguliwa mashtaka.

Mapema leo Jumatano waandamanaji wanaomuunga mkono na wanaompinga Yoonwalikusanyika karibu na makazi ya kiongozi huyo wakizozana  baada ya mahakama kutoa waranti nyingine ya kumkamata kiongozi huyo ambaye aliiingiza nchi hiyo katika machafuko ya kisiasa mwezi uliopita kwa tamko la kuanzisha sheria ya kijeshi na tangu wakati huo amejificha katika makazi ya rais na kugoma kuitikia wito wa kwenda kuhojiwa na timu ya wachunguzi.

Oh Dong-woon, Mkuu wa Ofisi ya Uchunguzi wa kesi za Ufisadi kwa Viongozi wa Vyeo vya Juu (CIO) ambayo inaongoza uchunguzi huo dhidi ya Yoon ameomba radhi kwa kushindwa kwa jaribio la kukamatwa Yoon Ijumaa iliyopita baada ya mvutano mkali wa karibu saa sita katika makazi ya rais mjini Seoul.