Rais Yoon hatohudhuria kesi dhidi yake kwa sababu za usalama
12 Januari 2025Rais wa Korea Kusini aliyeondolewa madarakani na bunge Yoon Suk Yeol, hatohudhuria kikao cha kwanza cha kesi dhidi yake wiki ijayo kwa sababu za kiusalama.
Mahakama ya katibaimepanga tarehe za kusikiliza kesi hiyo kuanzia Januari 14 hadi Februari 4. Hata hivyo wakili wa kiongozi huyo amesema rais Yoon yuko tayari kujitokeza mahakamani, ikiwa masuala ya usalama yatashughulikiwa.
Yoon, amekuwa akizuiliwa katika makazi ya rais na kulindwa na kikosi cha walinzi tangu aliposimamishwa kazi mwezi uliopita, kufuatia tangazo lake la muda mfupi la sheria ya kijeshi ambalo liliitumbukiza nchi hiyo katika machafuko ya kisiasa.
Amekataa kukutana na waendesha mashitaka na wachunguzi, na mapema mwezi huu kikosi chake cha walinzi kilizuia jaribio la kumkamata kufuatia mvutano uliodumu kwa masaa kadhaa.