Rais wa Colombia ashinda tuzo ya Nobel
7 Oktoba 2016Rais wa Colombia Juan Manuel Santos ndiye mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2016.
Ametunukiwa tuzo hiyo kufuatia juhudi zake za kuendeleza mchakato wa kuhimiza amani nchini mwake, hasa ikizingatiwa nchi hiyo ya Amerika ya Kusini imeshuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka 50.
Juan Manuel Santos, ambaye ni rais wa Colombia alianzisha mazungumzo yaliyochangia maridhiano kati ya serikali ya Colombia na wapiganaji wa FARC, na kuendeleza mchakato huo. Kamati hiyo ya watu wa tano ya Nobel yenye makao yake makuu Oslo nchini Norway ikiongozwa na Kaci Kullman imesema hayo wakati ikimtangaza Juan Santos kuwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka huu 2016.
Kamati hiyo imeongeza kuwa "ushindi huo unapaswa kuwa heshima kwa raia wa Colombia na kwa wale waliochangia mchakato wa amani na wawakilishi wa waathiriwa wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe". Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Colombia vimesababisha vifo vya watu 220 000 na kusababisha watu milioni 6 kuyahama makaazi yao.
Hata hivyo ushindi wa Manuel Santos haukutarajiwa hasa baada ya raia wa Colombia kupiga kura ya kuupinga mkataba alioridhiwa na wapiganaji wa Kimaxi kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka 52. Licha ya kura hiyo Santos aliahidi kufufua mpango wa amani. Ni kutokana na juhudi hizo za rais Santos kamati ya Nobel mjini Oslow imesisitiza kuzitambua kama alivyoweka wazi mwenyekiti wa kamati hiyo Kaci Kullman.
Tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2016 ilivutia jumla ya wagombea 376. 228 wakiwa watu binafsi huku 148 yakiwa ni mashirika.
Miongoni mwa waliopigiwa upatu kutwaa tuzo hiyo yenye thamani ya dola laki tisa na elfu thelathini, ni wale walioafikia mkataba wa nyuklia kati ya Iran na nchi sita kuu za magharibi kwa lengo la kupunguza uwezo wa Tehran katika utumiaji wa nyuklia.
Kadhalika watoaji huduma wa kujitolea nchini Syria kwa jina White helmets sambamba na Raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, dakitari Denis Mukwege ambaye kwa mara nyingine aliteuliwa kwenye tuzo hiyo. Mukwege aliteuliwa kuwania tuzo hiyo kufuatia juhudi zake za kuangazia masaibu ya wanawake waliolengwa kwenye machafuko na hata kubakwa.
Tuzo ya amani ya Nobel ilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1901. Hadi leo jumla ya tuzo 130 zimetolewa, 104 ikikabidhiwa watu binafsi na 26 kwa mashirika.
Tuzo hii hukabidhiwa mtu ambaye amefanya kazi nzuri na muhimu kabisa katika jamii au miongoni mwa mataifa.
Mwandishi: John Juma/ DPE
Mhariri:Yusuf Saumu