Rais wa Chad afariki dunia
20 Aprili 2021Msemaji wa jeshi la Chad amesema Rais Idriss Deby amefariki dunia.
Kupitia matangazo ya televisheni ya umma wa taifa hilo, msemaji wa jeshi, Azem Bermendao Agouna amesema kwamba baraza la kijeshi limemchagua mtoto wa kiongozi huyo, Mahamat Kaka, kuwa rais wa mpito.
Tangazo la kifo chake limetokea saa chache tu baada ya Deby kutangazwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 79 ya kura licha ya wapinzani wake wakuu kuamua kususia uchaguzi huo wa Aprili 11.
Waziri mkuu wa zamani, Albert Pahimi Padacke ameshika nafasi ya pili katika kinyang'anyiro hicho kwa kupata asilimia 10.32 tu, na idadi ya waliojitokeza ilikuwa asilimia 64.81, kwa mujibu wa takwimu za awali zilizotangazwa na mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kodi Mahamat Bam.
Matokeo hayo yalitangazwa baada ya jeshi kufanya mazoezi kwenye mitaa ya mji mkuu, N'Djamena.
Kwa ushindi huo, Rais huyo mwenye umri wa miaka 68 angeiongoza nchi hiyo kwa muhula wa sita mfululizo.