Rais wa Afghanistan awavutia wawekezaji
28 Novemba 2018Katika siku ya kwanza ya mkutano kuhusu Afghanistan, Rais Ghani alizinadi sera za serikali yake ambazo zinanuia kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kurahisisha biashara, kuimarisha miundo mbinu na kuruhusu uwekezaji katika raslimali za nchi. "Ni Afghanistan iliyobadilika. tunakaribisha biashara. Natumai nanyi mnakaribisha ushirikiano. Ahsanteni" Alisema Ghani.
Halmashauri Kuu ya Ulaya iliahidi euro milioni 474 za msaada kwa Afghanistan ili kuyasaidia mageuzi ya sekta ya umma na kuyashughulikia masuala ya uhamiaji na kupoteza makazi. Ghani alitaja ukosefu wa usalama katika sentensi moja tu, bila kuyazungumzia mashambulizi makali ya kila mara yanayofanywa na Taliban na wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS ambayo ndio chanzo kikuu cha kukosekana utulivu nchini Afghanistan
Wakimbizi wamekuwa wakirejea nyumbani
Wakati akiyasifu mageuzi ya sekta ya usalama na vita dhidi ya ufisadi nchini Afghanistan, Toby Lanzer, naibu mkuu wa Ujumbe wa Misaada nchini Afghanistan UNAMA amesema watu milioni 3.6 kati ya milioni 35 nchini humo wanakabiliwa na njaa kutokana na kiangazi "kufikia sasa mwaka huu, watu 675,000 wamerejea Iran kutoka Iran na wakati huo huo, nusu ya watu milioni moja, wamelazimika kukimbia makazi yao nchini humo. kwa nini? kwa sababu ya machafuko yanayoendelea na kwa sababu ya kiangazi"
Zaidi ya watu 200,000 wameyakimbia maeneo yaliyokumbwa na kiangazi mwaka huu. Aidha, Ofisi ya Mratibu wa Masuala ya Kiutu ya Umoja wa Mataifa – OCHA inasema mapigano yanayoendelea yamesababisha watu 300,000 kupoteza makazi yao nchini humo tangu Januari.
Serikali inakabiliwa na changamoto kubwa kuweka udhibiti katika maeneo mengi atangu kumalizika operesheni ya NATO iliyoongozwa na Marekani mwaka wa 2014.
Marekani kuzungumza na Taliban?
Marekani imefanya mazungumzo ya awali na Taliban katika miezi ya karibuni kama hatua ya kwanza kuelekea mazungumzo kati ya wanamgambo hao na serikali ya Kabul, lakini Suraya Pakzad mwanaharakati wa haki za wanawake anasema ana wasiwasi kuhusu kuwapa Taliban jukumu katika serikali ya baadaye. Taliban ni wapinzani wakubwa wa usawa wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF, wasichana wamekuwa waathiriwa wa kiangazi cha mwaka huu, kwa sababu umaskini umezifanya familia nchini humo kuwauza watoto 261 wengi wao watoto kati ya Julai na Oktoba.
Karibu mawaziri wa kigeni 20 – akiwemo Sergei Lavrov wa Urusi na Heiko Maas wa Ujerumani – wanatarajiwa kuhudhuria siku ya pili ya kongamano hilo leo.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga