Urusi na Korea Kaskazini kuanzisha ushirikiano mkubwa.
18 Juni 2024Rais Vladmir Putin wa Urusi anayeanza leo ziara ya siku mbili Korea Kaskazini ameishukuru nchi hiyo kwa kuunga mkono hatua zake nchini Ukraine,na kuahidi kushirikiana na Pyongyang kwa karibu kukabiliana na vikwazo vya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.
Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kwamba barabara za mji mkuu wa Korea Kaskazini zimepambwa kwa mabango ya picha za rais Vladimir Putin na bendera za Urusi.
Saa chache kabla ya rais Vladmir Putin kuwasili Korea Kaskazini kituo cha taifa cha habari cha Korea Kaskazini kilichapisha taarifa ya kiongozi huyo wa Urusi inayosema kwamba nchi hizo mbili yaani Korea Kaskazini na Urusi zitashirikiana kukabiliana kikamilifu na kile alichokiita dhamira ya nchi za Magharibi za kutaka kuzuia kuanzishwa mshikamano wa mataifa usiokubali kuendeshwa na mfumo unaosimamiwa na taifa moja lenye nguvu.
Putin pia amesema nchi yake na Korea Kaskazini zitaanzisha mifumo ya kibiashara na kibenki ambayo haitodhibitiwa na mataifa ya Magharibi lakini pia kwa pamoja zitapambana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi zao.
Na zaidi, mataifa hayo mawili yatatanuwa ushirikiano kwenye sekta za utalii, utamadui na elimu.
Kiongozi huyo wa Urusi atakutana kwa mazungumzo na mwenzake Kim Jong Un huu ukiwa mkutano wao wa kilele katika ziara hiyo ya kwanza ambayo anaifanya Korea Kaskazini katika kipindi cha miaka 24.
Korea Kaskazini iko chini ya vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyopitishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na mpango wake wa kutengeneza silaha za Nyuklia pamoja na makombora wakati Urusi kwa upande mwingine pia inakabiliana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani pamoja na washirika wake wa mataifa ya Magharibi, kutokana na vita vyake vinavyoendelea huko Ukraine.
Kabla ya kuelekea Korea Kaskazini imeleezwa kwamba alipitia kwamba katika mji ulioko mashariki mwa Urusi wa Yakutsk,ambako alikwenda kuzungumza na gavana wa jimbo hilo na kuelezwa kuhusu maendeleo ya miradi inayohusu teknolojia na ulinzi.Soma Pia: Korea Kaskazini yakanusha kubadilishana silaha na Urusi
Ziara ya Putin Pyongyang,inakuja katika wakati kukiweko kiwingu cha wasiwasi unaoongezeka kuhusu kuwepo makubaliano ya Korea Kaskazini kuipatia Moscow silaha inazozihitaji sana kwaajili ya kuendeleza vita vyake Ukraine,na Urusi badala yake inaipatia Korea Kaskazini msaada wa kiuchumi na Teknolojia itakayosaidia kuimarisha mpango wake wa kutengeneza silaha za Nyuklia na makombora,ambayo bila shaka ni kitisho.
Na harakati hizi za kusaidiana kati ya Korea Kaskazini na Urusi zimeongezeka zaidi tangu Kim Jong Un alipoitembelea Urusi mwezi Septemba na kukutana na rais Putin kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019.
Baada ya ziara yake Korea Kaskazini Putin ataelekea Vietnam Jumatano 19 hadi 20.