1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Tshisekedi ziarani nchini Marekani akutana na Pompeo

Sylvia Mwehozi
4 Aprili 2019

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Felix Tshisekedi amekutana na baadhi ya mawaziri wa Marekani akiwemo waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo, na kuzungumzia ushirikiano baina ya nchi hizo.

https://p.dw.com/p/3GEH9
New York Besuch Kongo Präsident Felix Tshisekedi bei Pompeo
Picha: Getty Images/AFP/A. Caballero-Reynolds

Ziara hiyo ni ya kwanza nje ya bara la Afrika toka Felix Tshisekedi alipoapishwa kuwa rais wa Kongo. Mjini Washington, Rais Tshisekedi amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo, ambapo wamezungumzia masuala ya kisiasa, ulinzi na ya kiuchumi. Rais Tshisekedi amesema kwamba ziara yake inalenga kukuza hasa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Kongo na Marekani.

''Katika ushirikiano wetu, Kongo inataka kuimarisha uongozi wake wa utawala bora ambao utachangia pia kuimarisha sekta ya elimu na afya. Kwa hiyo ziara yangu ni kutaka hasa kuwepo na uhusiano wa kirafiki baina ya nchi zetu mbili. Tunataka ushirikiano ambao kila upande utafaidika'', alisema Tshisekedi.

Pompeo amempongeza Tshisekedi katika hatua yake ya kutaka mageuzi. Huku akielezea umuhimu wa Kongo kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji. Ikiwa hakukutarajiwa kusainiwa kwa mkataba wowote ule kwa sasa, lakini Marekani imeelezea kwamba Kongo inahitaji kupambana na rushwa ili kuwaruhusu wajasiriamali wa Kimarikani kuja kuwekeza Kongo.

Präsident des Kongos: Felix Tshisekedi
Rais Felix Tshisekedi akiwa mjini Addis Ababa hivi karibuniPicha: picture-alliance/AA/M. Hailu

Mbali na uhusiano wa kidiplomasia, rais wa kongo amehitaji pia ushirikiano kwenye sekta ya nishati na afya. Kwa hiyo alikutana siku ya Jumatano na Waziri wa Nishati Rick Perry. Kongo inahitaji umeme kwa ajili ya uchimbaji madini yake na huduma kwa jamii. Walimulika pia mradi wa ujenzi wa bwawa kubwa la umeme la INGA ambao unahitaji Dola bilioni 22.

Ingawa hatokutana na Rais wa Marekani Donald Trump, Rais Tshisekedi anatarajiwa kukutana pia na waziri wa ulinzi wa Marekani ambapo pamoja na mambo mengine watajadiliana kuhusu masuala ya kiusalama. Francois Balumuene, balozi wa Kongo nchini Marekani amesema kwamba Marekani inaweza kuchangia katika kumaliza kitisho cha makundi ya wapiganaji huko mashariki mwa Kongo.

''Kwa miaka mingi sasa Kongo ina matatizo ya kiusalama kwenye maeneo ya mashariki. Leo, maeneo hayo yamekuwa ngome ya wapiganaji wa kigeni ambao ni magaidi. Ni lazima tuhakikishe ukosefu wa usalama unamalizika nchini kwetu. Wamarekani wana uwezo wa kutuunga mkono ili kumaliza machafu hayo''.

Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Rais Tshisekedi anatarajiwa kukutana na viongozi wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF. Mashirika hayo yalisitisha rasmi ushirikiano wa kifedha na Kongo mnamo mwaka wa 2005 baada ya kuilazimisha Kongo kuandaa uchaguzi wa kidemokrasia. 

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo