1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump: Shambulio la Texas limetokana na tatizo la akili

6 Novemba 2017

Trump amesema kisa cha mtu aliyewaua watu 26 kwa kuwapiga risasi katika kanisa dogo la jimbo la Texas kilitokana na matatizo ya akili wala si mjadala kuhusu umiliki wa bunduki

https://p.dw.com/p/2n5Of
USA Texas Schießerei Kirche in Sutherland Springs
Picha: picture-alliance/AP Photo/Austin American-Statesman/N. Wagner

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa kisa cha mtu aliyewaua watu 26 na kuwajeruhi wengine 20 kwa kuwapiga risasi katika kanisa dogo la jimbo la Texas kilitokana na matatizo ya akili na  wala si suala la mjadala kuhusu umiliki wa bunduki. Trump ameyasema hayo akiwa ziarani  nchini Japan, sehemu ya ziara yake barani Asia .

Akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa habari mjini Tokyo, kuhusu sera anazoweza kuunga mkono kuhusiana na shambulizi la risasi ambalo limesababisha vifo vya watu 26 katika jimbo la Texas, Rais Trump amejibu kwa kusema kulingana na ripoti ya awali ya uchunguzi wa tukio hilo, mtu huyo aliyekuwa na bunduki alikuwa na matatizo ya akili. Trump ambaye yuko nchini Japan, kituo cha kwanza cha ziara ya siku 12 katika nchi tano za Asia, ameongeza kuwa nchi yake inakumbwa na wakati mgumu lakini suala la umiliki wa bunduki halipaswi kulaumiwa kuhusiana na kisa hicho.

"Ninafikiri ni tatizo la akili. Tuna matatizo mengi  ya akili katika nchi yetu kama ilivyo katika nchi nyingine, lakini hili halihusiani na suala la bunduki.  Kwa bahati mzuri  mtu mwengine alikuwa na bunduki upande wa pili na kufyatua risasi dhidi yake. Hili ni suala la tatizo kubwa la akili, ni tukio la kuhuzunisha sana. Ndivyo ninavyoiona mimi" Amesema Trump.

Mshukiwa wa shambulizi hilo apatikana amekufa

USA Texas Schießerei Kirche in Sutherland Springs
Picha: Imago/ZUMA Press/B. Owen

Tukio hilo la usiku wa kuamkia Jumapili , limejiri wiki tano tu baada ya shambulio baya zaidi la risasi katika histora ya Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Mtu huyo mwenye bunduki, aliwafyatulia risasi watu waliokuwa wakiingia kanisani, katika kanisa la Baptist eneo la Sutherland Springs, takriban kilomita 65 mashariki kwa San Antonio, kisha akaingia kanisani na kuendelea kuwapiga watu risasi, akawaua waumini walio na umri wa kati ya miaka 5 hadi 72.

Maafisa wameeleza kuwa mshambuliaji huyo ambaye ametambuliwa kwingi kwa jina la Devin Kelley, mzungu  mwenye umri wa miaka 26, alitoroka kwa kutumia gari lake baada ya kufyatuliwa risasi na raia aliyekuwa na bunduki. Baadaye alipatikana amekufa  katika kaunti jirani.

Haikubainika moja kwa moja ikiwa mshukiwa alijiua mwenyewe au kama alipigwa na risasi. Hayo yamesemwa na maafisa.

Jeshi la angani la Marekani limesema Kelley alihudumu katika kambi ya jeshi la New Mexico kuanzia mwaka 2010 kabla ya kupewa hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja na mahakama ya kijeshi baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga mkewe na mwanaye.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE
Mhariri: