Rais Samia athibitisha maambukizi ya Marburg nchini Tanzania
20 Januari 2025Akizungumza mjini Dodoma katika mkutano wa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO , Tedros Adhanom Ghebreyesus; Rais Samia amesema kuwa angalau kisa kimoja cha ugonjwa huo kimethibitishwa.
Katika tangazo lake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema vipimo vya kitaalamu vilivyofanywa katika Maabara ya Kabaile huko mkoani Kagera na baadaye kuthibitishwa jijini Dar es Salaam, vilithibitisha kuwa mgonjwa mmoja alikuwa ameambukizwa virusi vya Marburg.
Wiki iliyopita waziri wa afya wa Tanzania Jenista Mhagama alikuwa amekanusha kuwepo kwa ugonjwa wa nchini humo akisema hakuna mtu aliyepatikana na maambukizi ya virusi hivyo.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hii sio mara kwanza kwa mripuko wa Marburg kuikumbwa Tanzania baada ya mara ya kwanza kuibuka Machi 2023 katika mkoa wa Kagera.
Soma pia:Afrika CDC tayari kuisaidia Tanzania kudhibiti Marburg
Hayo aliyasema baada ya WHO kuarifu kuwa ilipokea ripoti za kuaminika kwamba hadi tarehe 10 Januari, watu wanane walikuwa tayari wamekufa mkoani Kagera, baada ya kuugua maradhi yenye dalili sawa na za ugonjwa wa Marburg.
Dalili hizo ni pamoja na maumivu ya kichwa, homa kali, maumivu ya mgongo, kuhara, kutapika damu, udhaifu wa misuli na kutokwa na damu.
Asilimia 88 ya watu wanaougua homa ya virusi vya Marburg wanakuwa na hatari ya kukutwa na mauti. Homa hiyo inafanana na ile ya Ebola, ambayo huambukizwa kwa binadamu kutoka kwa aina ya popo wanaopatikana katika maeneo mengi ya Afrika Mashariki.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake imeimarisha juhudi zake za kukabiliana na mlipuko huo na kwamba timu ya dharura tayari imetumwa katika eneo lililoathirika kufuatilia visa vyote vinavyoshukiwa na kujaribu kudhibiti mlipuko huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema shirika lake litatoa dola milioni 3 kutoka mfuko wake wa dharura kusaidia juhudi za kudhibiti mlipuko huo nchini Tanzania.
Soma pia:Rwanda yatangaza mwisho wa mlipuko wa kirusi cha Marburg