Sudan Kusini wajadili uwezekano wa kufanya uchaguzi Desemba
14 Agosti 2024Nchi hiyo changa zaidi duniani bado haijashiriki mchakato wa uchaguzi wa kidemokrasia ikiwa ni takribani miaka 13 tangu kile kinachoitwa uhuru wake uliopiganiwa kwa bidii kutoka kwa Sudan, hali ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa watu wake na jumuiya ya kimataifa.
Katika taarifa ambayo imechapishwakatika ukurasa wa Facebook wa ofisi hiyo ya rais inaeleza, "Rais, pamoja na viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa, wameazimia kutafuta ushauri wa kitaalamu kutoka kwa taasisi za uchaguzi kuhusu uwezekano wa kufanya uchaguzi ujao."
Mkutano huo ulitathmini hali ya kuyumba kwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano kati ya vikosi vinavyomtii Kiir na mpinzani wake mkuu ambaye sasa ni Naibu Rais Riek Machar.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wataka Sudan Kusini kufanya uchaguzi
Waziri mwenye dhamana na Masuala ya Baraza la Mawaziri la taifa hilo, Martin Elia Lomuro alisema mapitio hayo "yalilenga kutoa ratiba halisi kwa viongozi wa kisiasa kukubaliana kuhusu uchaguzi".
Lengo la makubaliano ya amani ya Sudan Kusini
Mkataba wa 2018 ulifungua njia kwa serikali ya mgawanyo wa madaraka na uliweka ramani ya muda wa mpito wa kisiasa na hatimae kuandaliwa uchaguzi.
Lakini itakumbukwa tu, Agosti 2022, viongozi wa Sudan Kusini walikubaliana kuongeza muda wa mpito kwa miezi mingine 24, hadi Februari 2025, na uchaguzi ukapangwa kufanyika Desemba 22 mwaka huu.
Hata hivyo, maeneo muhimu ya makubaliano hayo badohayajakamilika, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa katiba ya kitaifa na kuunganishwa kwa vikosi hasimu vya wapigani vya Kiir na Machar. Iwapo uchaguzi utafanyika pia unaweza kutegemea matokeo ya mazungumzo ya amani mjini Nairobi kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi ambayo hayakusaini mkataba huo wa 2018.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimeua zaidi ya watu 400,000
Taifa hilo limekuwa katika juhudi za kujikwamua kutokana na mzozo wa 2013-2018 uliosababisha vifo vya watu 400,000 na kuwafurusha mamilioni ya wengine katika makaazi yao, na bado linakumbwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, ghasia za kikabila, majanga ya mabadiliko ya tabia nchi na ufisadi.
Moja ya nchi maskini zaidi duniani licha ya utajiri mkubwa wa mafuta, uchumi wake umepata mkwamo baada ya kupata pigo lingine kufuatia bomba lake la mafuta kupasuka mwezi Februari katika eneo la taifa jirani la Sudan, iliyoko katika vita. Mkasa huo wa kupasuka kwa bomba la kusafirisha mafuta ulipelekea sarafu ya nchi hiyo kudorora na bei ya bidhaa za msingi kupanda.
Soma zaidi:Sudan Kusini: Hakuna Mafuta, hakuna chakula
Mwezi uliopita, shirika la kimataifa la hisani la Save the Children lilionya kwamba sehemu za nchi hiyo ziko kwenye "ukingo wa njaa" kwa sababu ya mafuriko wakati wa msimu wa mvua za wakati huu.
Chanzo: AFP