1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto aidhinisha sheria ya Tume ya Uchaguzi IEBC

Shisia Wasilwa
9 Julai 2024

Rais William Ruto wa Kenya ametia saini mswada wa marekebisho wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi nchini humo IEBC na kuwa sheria, huku akitaja hatua hiyo inalenga kuboresha mifumo ya kidemokrasia katika taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4i3VO
Nairobi, Kenya I Rais William Ruto
Rais William RutoPicha: Thomas Mukoya /REUTERS

Sheria hiyo mpya inatoa nafasi ya kuundwa upya kwa jopo ambalo litawapiga msasa mwenyekiti na makamishna sita wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya.

Hafla hiyo ilifanyika katika jumba la mikutano la kimataifa kinyume na utamaduni wa rais kutia sahihi miswada kuwa sheria katika Ikulu ya Nairobi.

Sheria hiyo miongoni mwa mambo mengine itaangazia nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi na wanachamana wake.

Aidha inaelezea mchakato wa kutengua na kuweka mipaka mipya ya maeneo mbali mbali ya taifa. Sheria hiyo ni matokeo ya mazungumzo ya ripoti ya kamati ya mazungumzo ya maridhiano ya taifa yaliyoongozwa na upande wa upinzani na serikali.

Soma pia:Chibukati atishia 'kumburuza' Raila mahakamani

Upande wa upinzani ulioongozwa na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka huku upande wa serikali ukiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichungwa. Rais Ruto amesema kuwa tume ya kusimamia uchaguzi ni nguzo muhimu kwa demokrasia ya taifa.

“Hatua ya leo inaashiria uwezo wa taifa wa kuyashinda masuala tata ambayo wakati mwingine hugawanya na kuathiri mshikamano na uthabiti wetu.”

Maeneo bunge kama vile Banissa hayajakuwa na mbunge tangu kuaga dunia kwa mbunge wao Kulow Hassan mwezi Machi mwaka uliopita sababu ya kuchelewa kuteuliwa kwa makamishna wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi nchini.

Shughuli muhimu za IEBC kusitishwa

Operesheni muhimu za tume ya IEBC zilisitishwa baada ya kustaafu kwa aliyekuwa mwenyekiti wake Wafula Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Mulu baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka sita.

Wagombea ugavana wapinga kuahirishwa kwa uchaguzi Mombasa

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amesema kutiwa saini kwa mswada huo ni hatua muhimu kwa taifa na kwamba iwapo mapendekezo yaliyoko kwenye ripoti ya mazungumzo ya maridhiano ya taifa yatazingatiwa taifa litaepuka machafuko ambayo yamekuwa yakishuhudiwa. Aidha ameongeza kusema kuwa utendakazi wa tume ya IEBC mwaka 2022 uliliaibisha taifa.  

“Tupo mahali muhimu sana katika historia ya taifa. Taifa limepiga hatua lakini pia kufeli kwenye nyanja nyingine. Ningependa kumfahamisha Rais, sasa tunahitaji mazungumzo mapana ya taifa.”

Soma pia:Wakili asema Chebukati ni mwathiriwa wa ''tetesi za wongo''

Kwa mujibu wa katiba, tume ya IEBC inastahili kuwa na mwenyekiti na wanachama wengine sita. Rais anatarajiwa kubuni jopo lenye watu saba kwa lengo la kuteua mwenyekiti na makamishna wa tume yenyewe.

Jopo hilo linastahili kuwa na wanaume wawili na wanawake wawili waliochaguliwa na Tume ya Idara ya Bunge, Chama cha Wanasheria nchini Kenya kitateua mtu mmoja sawa na Baraza la Dini nchini Kenya.

Rais amekuwa akishinikizwa kutia saini mswada huo na upinzani na vijana ambao wamekuwa wakiandamana wakitaka uongozi bora.