1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Nicolas Sarkozy apendekeza kuwa msuluhishi kati ya Wayahudi na Wapa...

Nijimbere, Gregoire23 Juni 2008

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amesema mbele ya bunge la Israel kwamba anaweza kuwa msuluhishi na kuwasaidia Wayahudi na Wapalestina kufikia mkataba wa amani.

https://p.dw.com/p/EPYs
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: AP

Katika hotuba yake mbele ya bunge la taifa la Israel mjini Jerusalem, ya kwanza ya kiongozi wa Ufaransa tangu ile ya Francois Mitterand mwaka 1982, rais Nicolas Sarkozy, amesema “Ufaransa iko tayari kutoa dhamana yake, wanadiplomasia, mbinu na wanajeshi kufanikisha juhudi za kusaka amani kati ya Wayahudi na Wapalestina“, kabla ya kuongeza “mnaweza kuiamini Ufaransa“.

Tangu kuchukuwa madaraka kiasi cha mwaka mmoja uliopita, rais Nicolas Sarkozy alisema yeye ni rafiki wa Israel na kwamba hakuwezi kuwa na mabishano kuhusu usalama wake. Hata hivyo ameikosoa Israel kwa kusema kuwa amani haiwezekani bila nchi hiyo kusimamisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi mashariki mwa Jerusalem na wale walioko katika maeneo ya ukingo wa magharibi mwa mto Jordan wahamie Israel baada ya kupewa fidia. Na itabidi mji wa Jerusalem utambuliwe kama mji mkuu wa taifa zote mbili yaani Israel na Palestina. Rais Sarkozy, yeye anaamini mkataba wa amani kati ya Israel na wapalestina unaweza kufikiwa siku za usoni.


Afisa mmoja wa karibu na rais Sarkozy, amesema kuwa vuguvugu la uchaguzi nchini Marekani, limetoa nafasi kwa wanasiasa wengine kuhusika zaidi na swala hilo la amani ya mashariki ya kati. Isitoshi ziara hiyo ya rais Nicolas Sarkozy inaweza kutafsiriwa na watu kuwa Umoja wa Ulaya unaksudia kuchukuwa jukumu kubwa katika kuusuluhisha mgogoro wa mashariki ya kati wakati Ufaransa itachukuwa usukani wa kuungoza Umoja huo julai mosi.


Akizungumza juu ya Iran, rais Nicolas Sarkozy, amesema nchi yake iko pamoja na Israel kupambana na ugaidi duniani na kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ni jambo lisilokubalika kwa Ufarsana.

Umoja wa Ulaya una wasi wasi juu ya mpango huo wa nyuklia wa Iran na ikiwa nchi hiyo itatengeneza silaha za nyuklia, Ufaransa itapinga kwa kila njia, amesema rais Sarkozy ambae amependekeza kuweko na majadiliano juu ya kile amekitaja kuwepuka janga aidha kwa Iran kupata bomu la nyuklia au kutokea shambulio dhidi ya nchi hiyo. Umoja wa Ulaya ambao utaongozwa na rais Nicolas Sarkozy kuanzia tarehe mosi Julai, unatarajia kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya Iran kama shinikizo ili nchi hiyo itekeleze mwito wa jumuiya ya kimataifa.

Israel imekwishaanza mazungumzo na Syria lakini mafisa wanasema hakuna hatua imeshapigwa kuweza kuzungumziwa kati ya waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa Syria Bashar al-Assad katika mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterranea mjini Paris mwezi ujao.