Rais Ndayishimiye awakaribisha wawekezaji Burundi
19 Septemba 2020Serikali ya Burundi imeihakikishia Jumuiya ya Afrika mashariki kuwa nchi yao iko salama na inawakaribisha wawekezaji katika sekta mbalimbali kwenda kufanya biashara na nchi hiyo ambayo imekuwa katika machafuko ya kisiasa na kikabila kwa zaidi ya muongo mmoja.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Burundi, Everiste Ndayishimiye, alipoitembelea Tanzania kwa ziara ya siku moja ambapo alikutana na Rais wa Tanzania, John Magufuli katika mji wa Kigoma magharibi mwa Tanzania.
Rais Ndayishimiye amebainisha kuwa baada ya kumalizika uchaguzi uliofanyika kidemokrasia, serikali yake ilikaa na pande zote za kisiasa na kukubaliana kuhakikisha nchi haiendelezi migogoro, sambamba na kufuta dhana za makabila ya watutsi na wahutu na kukubaliana kuwa Burundi ina kabila moja tu ambalo ni warundi.
"Sisi ni warundi, tunazungumza lugha moja, hakuna sababu ya kuendelea kutambua makundi ya wahutu na watutsi kama makabila, kabila letu ni warundi na lugha yetu ni Kirundi. Wazungu walitumia ukabila kutugawanya ili kututawala, sasa tunajitambua kama taifa huru,” alisema rais Ndayishimiye
Aidha Burundi kupitia kwa rais wake imeishukuru Tanzania kwa kuendelea kuwahifadhi wakimbizi wa Burundi sambamba na kuwapatia uraia wale waliopenda kubaki Tanzania baada ya kuishi kwa miaka 40 ambapo Tanzania ilitoa vyeti vya uraia kwa wakimbizi wapatao laki moja na sitini elfu waliokuwa katika kambi na makazi ya Mishambo, Katumba na Ulyankulu katika mikoa ya Katavi na Tabora.
Amepongeza pia kuwepo kwa mkakati wa kuunganisha Burundi na mfumo wa usafiri wa anga, majini na nchi kavu kwa njia ya reli inayotarajiwa kujengwa kutoka Uvinza Tanzania hadi makao makuu ya nchi ya Burundi, Gitega.
Akihutubia wananchi wa mji wa Kigoma rais Ndayishimiye alisema Tanzania ni mzazi wa Burundi na kwamba udugu uliopo ni wa kihistoria na unatakiwa uanze kutumika katika ukuzaji wa uchumi na kuimarisha usalama kwa pande zote mbili, huku akisisitiza watanzania kuwaamini warundi.
Mahusiano ya Tanzania na Burundi
Kwa upande wake rais Magufuli amebainisha kuwa mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi yamekua zaidi huku akitaja kuwa thamani ya biashara kati ya mataifa hayo imeongezeka kutoka bilioni 115.15 mwaka 2016 hadi kufikia bilioni 201 mwaka 2020.
Ameongeza kuwa kituo cha uwekezaji cha taifa kimesajili miradi 16 kutoka Burundi yenye thamani ya shilingi bilioni 29 na kwamba makampuni makubwa 10 kutoka Tanzania yamefungua matawi nchini Burundi.
Kutokana na Burundi kutopakana na bahari, Tanzania imekuwa kitovu cha kiuchumi kwa nchi za maziwa makuu ambapo Burundi pekee hupitisha zaidi ya tani 481,000 kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda nchini humo.
Miradi kuanzishwa
Rais Magufuli amebainisha kuwa Tanzania imekubaliana na Burundi kujenga mtambo wa kisasa wa kuchenjua madini pamoja na Burundi kuuza madini yake katika soko la madini la mkoani Kigoma.
Tanzania imetaja pia kuanzishwa kwa miradi ya kimkakati kujenga reli ya kisasa kutoka Uvinza hadi Gitega, Burundi, kuboresha usafiri katika ziwa Tanganyika kwa kununua meli mpya mbili na kukarabati meli kongwe ya MV Liemba yenye umri wa zaidi ya miaka 100.
Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya rais Ndayishimiye nje ya nchi tangu alipoapishwa kuwa rais wa jamhuri ya Burundi mwezi Julai mwaka 2020.
Mwandishi: Prosper Kwigize