Rais Mwinyi akamilisha safu yake ya mawaziri Zanzibar
4 Machi 2021Kutoka chama cha ACT ni walioapicha ni Nassor Ahmed Mazrui ambaye ni mfanyabiashara na mwanasiasa aliyewahi kuhudumu katika serikali iliyotangulia mwaka 2010 hadi 2015 ambaye anachukua nafasi ya waziri wa Afya, ustawi wa jamii, wazee, wanawake na watoto, na Omar Said Shaaban, mwanasheria kitaaluma, ambaye anashika nafasi yajuu serikalini kwa mara ya kwanza.
Mwengine ni Dk Saada Mkuya Salum ambaye ni waziri wa nchi ofisi ya makamo wa kwanza wa rais, Mkuya aliyewahi kuwa waziri wa fedha katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya utawala wa Dk Jakata Mrisho Kikwete.
Muda mfupi baada ya kiapo mawaziri hao walizungumza na waandishi wa habari na kuelezea majukumu yao. Nassor Mazrui alisema wizara yake ni kubwa inayotegemewa na watu wote katika kufikia malengo hivyo amejipanga kwenda kufanya kazi.
Sera ya uchumi wa bluu ambao sasa unapigiwa debe na awamu hii ya nane itahitaji viwanda hivyo waziri wa wizara hiyo Omar Said Shaaban ameahidi kuimarisha viwanda kwa kutumia malighafi zilizopo nchini ili Zanzibar irudi katika hadhi yake.
Kwa upande wake Sada Mkuya amesema wizara yake inashughulikia mambo mtambuka na atamsaidia makamo wa kwanza wa rais kutafuta majibu ya changamoto za madawa ya kulevya, Ukimwi na kuhifadhi mazingira.
Wakati huo huo katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini Rais Mwinyi pia amemuapisha Kamishna mpya wa mapato Salum Yussuf Ali ambaye ameahidi kuzipa miaya ya ukwepaji wa kodi nchini.
Kuapishwa kwa mawaziri hao kunakamilisha safu ya baraza la mawaziri na kufikia kumi tano kama Dk Mwinyi alivyoamua kulifanya baraza lake liwe dogo ili kupunguza matumizi.
Sasa Jicho na masikio ya wananchi wanalekezwa kusubiri uteuzi wa watendaji ambao ni wakurugenzi, wakuu wa idara na mashirika na taasisi za umma.