1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Lukashenko ashinda uchaguzi nchini Belarashia

Josephat Charo20 Machi 2006

Tume ya uchaguzi nchini Belarashia imemtangaza rais Alexander Lukashenko kama mshindi wa uchaguzi nchini humo. Lukashenko amejipatia asilimia 82.6 ya kura zote na kumshinda mpinzani wake mkuu Alexander Milinkevich aliyepata asilimia sita pekee. Upinzani unailaumu serikali kwa wizi wa kura na udanganyifu.

https://p.dw.com/p/CHLc
Wafuasi wa Milinkevich wakiandamana mjini Minsk
Wafuasi wa Milinkevich wakiandamana mjini MinskPicha: AP

Akijulikana na mataifa ya magharibi kama dikteta wa mwisho barani Ulaya na ambye mienendo yake inachunguzwa kwa makini na Urusi, rais Alexander Lukashenko ameshinda uchaguzi wa Belarus na kuendelea kuhifadhi madaraka yake katika taifa hilo la muungano wa zamani wa Sovieti.

Uchaguzi wa jana Jumapili umemuwezesha Lukasheko kushinda awamu ya tatu kama rais wa Belarashia, lakini maelfu ya waandamanaji waliandamana katika uwanja wa Minsk wakiitikia mwito wa wanasiasa wa upinzani wanaotaka matokeo ya uchaguzi huo yafutiliwe mbali wakidai kulikuwa na udanganyifu.

Matokeo ya mwisho yalitangazwa saa chache baada ya waandamanaji takriban elfu 10 kukusanyika katika uwanja wa Oktoba mjini Minsk huku kukiwa na theluji, katika maandamano ambayo hayajawahi kufanyika katika miaka ya hivi karibuni. Rais Lukashenko alikuwa ameapa kuikata shingo ya mtu yeyote atakayejaribu kuvunja sheria na kuzusha ghasia lakini polisi hawakuchukua hatua yoyote.

Viongozi wa upinzani nchini Belarashia wanalalamika wakisema kampeni zao zilishuhudia kukamatwa na kutishwa kwa wafuasi wao. Mpinzani mkuu wa rais Lukashenko, Alexander Milinkevich, aliwaongoza wafuasi wake katika maandamano hayo huku wakiwa wameshika mabango yalisosema, ´Tunaamini, tunaweza, tutashinda´. Amewahimiza wafuasi wake wakusanyike tena kufanya maandamano mengine leo usiku.

Milinkevich bado anashikilia amemshinda rais Lukashenko kwa wingi wa kura. Anasema wananchi wa Belarashia hawamuogopi rais Lukashenko na lengo lao wanataka uchaguzi mwingine ulio huru na wa haki ufanyike. Mwito wa Milinkevich unakumbusha matukio yaliyotokea katika jamhuri za muungano wa zamani wa Sovieti za Georgia na Ukraine, ambako watetezi wa upinzani waliongoza maandamano makubwa kupinga matokeo ya uchaguzi waliyodai yalikuwa ya uongo.

Katika mataifa yote mawili viongozi waliokuwa wametangazwa washindi waliondolewa madarakani na nafasi yao kuchukuliwa na viongozi wa upinzani wanaoegemea mataifa ya magharibi.

Rais Lukashenko amejilimbikizia madaraka wakati wa utawala wake wa miaka 12, jambo lililomfanya rais George W Bush wa Marekani kuitaja Belarus kama taifa la pekee lenye utawala wa kiimla barani Ulaya. Hata hivyo Lukashenko bado anaungwa mkono na raia wengi wa Belarashia wanaoishi katika maeneo ya mashambani wanaosema kiongozi huyo amewaepusha mbali na mateso, maisha magumu na ubepari unaoendelea kushamiri katika mataifa mengi yaliyokuwa katika muungano wa zamani wa Sovieti.

Uchaguzi wa Belarashia unatarajiwa kuwa mada kuu katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya mjini Brussles Ubelgiji hii leo. Umoja wa Ulaya umeapa kuadhibu vitendo vya wizi wa kura kutumia vikwazo kama vile kufutilia mbali visa za kusafiria za maafisa waliohusika katika wizi huo.

Ikiwa ushahidi utadhihirisha kulikuwa na wizi wa kura, mawaziri wa umoja wa Ulaya huenda wakubaliane juu ya orodha ya maafisa wa serikali ya Belarashia watakaopigwa marufuku kutosafiri Ulaya katika majuma machache yajayo.