Rais Jacob Zuma awabinya Tsvangirai na Mugabe wamalize tofauti zao
18 Machi 2010Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kwa siku ya pili amefanya mazungumzo ya pamoja na viongozi wanaopingana nchini Zimbabwe akiwatia mbinyo wamalize tofauti zao na kuelekeza juhudi zao katika kuelekea uchaguzi mpya.
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma yuko nchini Zimbabwe katika siku yake ya pili ya ziara yake nchini humo
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na waziri mkuu Morgan Tsvangirai waliunda serikali ya umoja wa kitaifa mwaka mmoja uliopita lakini bado wamegawika juu ya masuala kadhaa ambayo yamekwamisha kuendelea kwa hatua ya kueleka katika uchaguzi mkuu mpya,hatua ambayo ni mojawapo ya mambo muhimu yaliyotajwa katika makubaliano yaliyotiwa saini na pande zote mbili.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amefanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wote wawili kwa pamoja baada ya hapo jana kukutana nao mbali mbali .
Kwa upande wake rais Mugabe amesema mazungumzo ya jana yalikwenda vizuri kama kawaida wakati Tendai Biti katibu mkuu wa chama cha Movement for Demokratic Change MDC cha bwana Tsvangirai akisema ni mapema mno kuzungumzia chochote kuhusu mkutano huo,isipokuwa cha muhimu ni ni kutoa nafasi ya kuyatatua masuala ambayo ni kizingiti katika mchakato mzima wa kufikia suluhisho kamili la kisiasa nchini Zimbabwe.
Kiongozi wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai hata hivyo analalamika kwamba rais Mugabe amejichukulia hatua ya kufanya uamuzi peke yake katika kuwateua maafisa wa ngazi za juu serikalini na pia kuendelea kuwakandamiza wafuasi wa chama hicho ikiwa ni pamoja na kukamatwa maafisa wake na kushtakiwa.
Msemaji wa rais Zuma Vincent Magweya akizungumza na shirika la habari la AFP alisema mazungumzo ya ana kwa ana pamoja na Mugabe na Tvangirai hapo jana yameonekana kutia moyo kwa maana ya kwamba rais Zuma amepata mtazamo kwamba pande zote mbili ziko tayari kuendelea mbele kufikia suluhisho la kudumu. Aidha Zuma amekutana pia na mwanasheria mkuu Johannes Tomana na gavana wa benki kuu Gideon Gono wote wakiwa ni kutoka kambi ya Tvsangirai.
Kadhalika jana usiku alifanya mazungumzo na Roy Bennett mweka hazina wa chama cha Mdc na ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini kufuatia madai ya kuhusika na njama dhidi ya Mugabe.
Pande zote mbili nchini Zimbabwe zinakabiliwa na shinikizo la kuzitaka zimalize tofauti zao na kutazama suala la kuandaa katiba mpya ambayo inatarajiwa kufungua njia ya kufanyika uchaguzi mpya.
Chini ya makubaliano ya kugawana madaraka ,iliwekwa wazi kwamba nchi hiyo inahitaji kuwa na katiba mpya itakayolazimika kupelekwa kwa wananchi waipigia kura ya maoni kufikia mwezi wa Novemba mwaka 2010 na kufungua njia hatimae ya kufanyika uchaguzi mpya kufikia mwezi Februari mwaka 2011.
Mashauriano juu ya katiba hiyo mpya yalitakiwa kuanza miezi tisa iliyopita lakini hilo halijafanyika na badala yake yanatarajiwa kuanza mwezi wa Aprili-
Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE
Mhariri AbdulRahman,Mohammed