1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump amfuta kazi John Bolton

11 Septemba 2019

Rais wa Marekani Donald Trump amemfuta kazi mshauri wa usalama wa kitaifa John Bolton kwa kukosa kuelewana naye kuhusu jinsi ya kushughulikia masuala ya Iran, Afghanistan na changamoto nyingine nyingi za kimataifa.

https://p.dw.com/p/3PNvc
John Bolton
Picha: picture-alliance/dpa/E. Vucci

Hatua hiyo ya Jumanne iliadhimisha hatua ya hivi punde ya kuondoka kwa sauti kuu ya upinzani katika mzunguko wa watu walio na ukaribu na rais Trump huku rais huyo mara nyingi akionekana kupinga ushauri unaokinzani na fikra zake. Hatua hii pia inajiri wakati wa majaribio makubwa kwa Trump katika masuala ya kimataifa huku akikabiliwa na maamuzi magumu kuhusu masuala magumu ya sera za kigeni.

Viongozi mbali mbali wametoa maoni yao kuhusiana na habari hizo ambazo hazikutarajiwa. Kulingana na Seneta Marco Rubio wa chama cha Republican ambaye ni mwanachama katika kamati ya seneti ya uhusiano wa mambo ya nje amesema kuwa amefanya kazi vizuri na Bolton na kwa maoni yake alitekeleza wajibu wake vyema lakini huo ni uamuzi wa rais aliye na haki ya kuchagua watu anaotaka kufanya kazi naye.

Shirika la habari la RIA limemnukuu naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov akisema leo kwamba Urusi haitarajii uhusiano wake na Marekani kuimarika mara moja kufuatia kuondoka afisini kwa John Bolton. Ryabkov amesema hatua kama hizo za mabadiliko nchini Marekani hazijasaidia uhusiano kurejea katika hali ya kawaida katika siku zilizopita.

Tangu kujiunga katika uongozi wakati wa msimu wa masika mwaka jana, Bolton ameonyesha pingamizi zake kuhusu hatua za rais dhidi ya Korea Kaskazini na hivi karibuni amekuwa mkosoaji wa ndani wa uwezekano wa mazungumzo kati ya Trump na viongozi wa Iran na kundi la Wataliban nchini Afghanistan.

Siku ya Jumanne kupitia mtandao wa twitter, Trump na Bolton walitoa habari zilizokinzana kuhusu kuondoka kwa Bolton afisini. Rais Trump alindika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba alimwambia Bolton Jumatatu usiku kwamba huduma zake hazihitajiki tena katika ikulu ya white house na Bolton akawasilisha barua ya kujiuzulu Jumanne asubuhi.

Lakini Bolton akajibu kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba ni yeye mwenyewe aliyetaka kujiuzulu siku ya Jumatatu na rais Trump akamwambia, ''tuzungumzie swala hili kesho.'' Rais Trump amesema kuwa atamtangaza atakayechukuwa nafasi hiyo ya mshauri wa masuala ya usalama wa kitaifa wiki ijayo.