Rais Trump aiondowa Marekani kutoka WHO kwa mara ya pili
21 Januari 2025Trump amechukuwa hatua hiyo, baada ya kuapishwa kurudi madarakani kwa muhula wa pili wa miaka minne. Amesema Marekani imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa shirika hilo.
''Sisi tulikuwa tunatowa dola milioni 500 kwa WHO wakati nilipokuwa hapa,na nikaiondowa Marekani kwenye shirika hilo. China ambayo ina wakaazi bilioni 1.4 , na sisi tuna milioni 350, kimsingi hakuna anayejuwa idadi yetu kwasababu kuna wahamiaji wengi haramu walioingia hapa. Lakini acha tuseme tuko milioni 325 na wao wana wakaazi bilioni 1.4. Wao wanalipa dola milioni 39. Sisi tunalipa dola milioni 500. Kwangu mimi hiyo sio haki,'' alisema Trump.
Trump aiondoa Marekani kwenye mkataba wa mazingira wa Paris 2015
Hatua hiyo ya Trump ya kuiondowa Marekani,kutoka WHO imewatia wasi wasi wanasayansi wengi wakikhofia huenda ikarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa miongo kadhaa katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kama vita Ukimwi,Malaria na Kifua Kikuu.
Waatalamu pia wametahadharisha juu ya hatua hiyo kwamba inaweza kudhoofisha mapambano dhidi ya magonjwa hatari ya miripuko yanayoweza kuchochea majanga.