1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Deby atakiwa kujiondoa katika uchaguzi wa 2024

Saleh Mwanamilongo
18 Januari 2024

Upinzani Chad umemtaka rais wa mpito Mahamat Idriss Deby Itno, ambaye alichukua madaraka mara baada ya kifo cha babake mwaka 2021, kujiondoa katika uchaguzi unaotarajiwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4bQMG
Mahamat Idriss Déby Itno
Rais wa Chad ​​​​Mahamat Idriss Déby ItnoPicha: Denis Sassou Gueipeur/AFP/Getty Images

Upinzani mkuu na kundi la mashirika ya kiraia la Wakit Tamma viliishutumu jumuiya ya kimataifa na Ufaransa hasa, kwa kuunga mkono kile walichosema kuwa ni urithi wa kifalme nchini Chad na kuunga mkono nia ya jenerali Mahamat Deby ya kunyang'anya mamlaka, ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu.

Upinzani umesema kuteuliwa kwa Mahamat kama mgombe urais ni njama dhidi ya katiba ya Chad. Béral ​​Mbaikoubou, mbunge wa upinzani katika Bunge la Mpito amesema uteuzi huu ni mwendelezo wa kimantiki wa mpango ulioratibiwa kwa ustadi na jeshi pamoja na chama cha MPS cha hayati rais Deby Itno.

"Tuna ushahidi hapa kwamba kila kitu tulichoambiwa baada ya kifo cha rais Deby, kwamba wanajeshi walilazimika kuchukua madaraka kwa ajili tu za utulivu na usalama kwa sababu nchi ilikuwa hatarini, yote haya yanaonekana leo kama mzaha kutoka dakika za kwanza za kutoweka kwa Rais Idriss Déby Itno. Leo, tunaposonga mbele, vinyago vinaanguka na njama hii inadhihirika wazi siku baada ya siku, " alisema Biral.

Upinzani na makundi yenye silaha yalisusia mazungumzo ya kitaifa yaliyoitishwa na uongozi wa kijeshi Agosti 2022. Mnamo Oktoba 2022, kati ya vijana 100 na 300 waliokuwa wakiandamana kwa amani kupinga kurefushwa kwa serikali ya mpito waliuawa kwa kupigwa risasi huko N'Djamena na vikosi vya usalama, kulingana na upinzani na mashirika ya kujitegemea.

Vyanzo hivyo vilisema zaidi ya watu  wengine 1,000 walifungwa kabla ya kusamehewa, huku wengine kadhaa wakiteswa au kutoweka. Mwishoni mwa Desemba 2023 katiba mpya ilipitishwa kwa asilimia 86 ya kura za ndio, licha ya upinzani kususia.

Deby aidhinishwa rasmi kugombea urais kupitia chama cha MPS

Mahamat Idriss Deby
Deby aidhinishwa rasmi kugombea urais kupitia chama cha MPSPicha: Gonzalo Fuentes/REUTERS

Mahamat Deby sasa ameidhinishwa rasmi kugombea urais na chama cha babake cha Patriotic Salvation Movement (MPS). Mahamat Zen Bada, Katibu Mkuu wa chama cha MPS amesema jenerali Mahamat Deby ni chaguo la busara.

Upinzani umesema ni jukumu la kizalendo kwa rais Mahamat Deby kukataa uteuzi huo ili kuinusuru demokrasia ya Chad. Upinzani na kundi la mashirika ya kiraia ya Chad Wakit Tama vilishutumu Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Chad, kwa kuingilia kati masuala ya ndani ya Chad kakika kile walichosema ni  mfumo wa mpango mkubwa wa kisiasa na kihimla wa Ufaransa katika eneo la Sahel.

Mkuu wa jukwaa la upinzani la Chad , GCAP, Max Kemkoye, alitoa wito wa kuweko na upinzani mkuu dhidi ya hatua ya rais Mahamat Deby kuwa mgombea wa uchaguzi na kupinga katiba mpya.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 37 alitangazwa kuwa mkuu wa kikosi cha kijeshi miaka miwili iliyopita baada ya waasi kumuua babake Idriss Deby Itno ambaye alichukua mamlaka katika mapinduzi na kulitawala taifa hilo la jangwani kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu.

Jumuiya ya kimataifa ilikuwa imemhimiza Mahamat Deby kutekeleza ahadi zake ya kuitisha uchaguzi ndani ya miezi 18 na kuachia madaraka kwa viongozi wa kiraia. Lakini rais mpya aliongeza miaka mingine miwili ya mpito na hivi sasa analenga kugombea uchaguzi wa baadae mwaka huu.