Rais Bouteflika wa Algeria kuwania muhula wa tano wa uraisi
12 Februari 2019Rais Abdelaziz mwenye umri wa miaka 81 amepuuzilia mbali wasiwasi wa kisiasa kutoka kwa wapinzani na makundi ya haki yanayopinga azma yake hiyo na kuitaja kama uongozi wa mkono wa chuma.
Rais huyo anayetumia kiti cha magurudumu na aliye na shida ya matamshi baada za kuugua kiarusi mwaka 2013 hapo jana alisema atawania muhula mwengine wa tano licha ya kwamba hana nguvu tena za kimwili kama awali.
Kituo cha habari cha Algeria kilimnukuu rais huyo akisema kwamba hamu yake kubwa ya kuongoza taifa hilo haijamwishia na ndio inampa ari na nguvu zaidi ya kushinda vikwazo anavyopitia kutokana na hali yake ya kiafya ambayo mtu yoyote inaweza kumkumba.
Siku ya Jumamosi (09.02.2019) chama kinachoongoza National Liberation Front, FNL, kilimtangaza Bouteflika kuwa mgombea wao wa kiti hicho cha uraisi kwa muhula wa tano.
Nchini Algeria anaheshimika sana kwa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya waasi wa kiisilamu na jeshi katika mataifa ya Afrika ya Kazkazini vilivyodumu kwa muongo mmoja ambapo watu laki mbili walifariki.
Bouteflika hakuathiriwa na vuguvugu la mageuzi
Bouteflika ni rais wa pekee wa Afrika ya Kazkazini aliyesalimika na vuguvugu la mageuzi la nchi za kiarabu ambapo katika taifa lake hakukuwa na maandamano baada ya kuwaahidi wananchi wake mabadiliko na nyongeza ya mishahara kupitia pato la mafuta.
Ila hivi karibuni uchumi wa taifa hilo umekuwa dhaifu kutokana na kushuka kwa bei za mafuta jambo linalolazimisha serikali kubana matumizi.
Chama kikuu cha kijamaa ambacho ni chama cha upinzani cha zamani, mwezi uliopita kiliitisha mkutano wa kukagua kikamilifu na uwezekano wa kususia uchaguzi huo na kusema hawatakuwa na mgombeaji.
Rais Buteflika ameahidi kutekeleza mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kupitia maridhiano iwapo atachaguliwa tena.
Wapinzani wake wakuu ni aliyekuwa waziri mkuu Ali Benflis, Generali mstaafu Ali Ghediri na kiongozi wa Chama Cha Waisilamu wenye Msimamo Wastani Abderazak Makri.
Rais Bouteflika alishinda uchaguzi wa mwaka 2014 kwa asilimia 81 ya kura licha ya kutofanya kampeni na kupiga kura akiwa katika kiti cha magurudumu.
Mwandishi: Faiz Musa Abdallah/AFPE
Mhariri: Josephat Charo