Rais Biden kuzuru Israel kwa mazungumzo na Netanyahu
17 Oktoba 2023Ziara hiyo ya Rais Joe Biden wa Marekani nchini Israel siku ya Jumatano imetangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken leo Jumanne.
Blinken amesema Rais Biden atathibitisha tena uungwaji mkono thabiti wa Marekani kwa Israel na kujitolea kwa Marekani kwa usalama wa Israel.
Blinken ameongeza kuwa Israel ina haki na wajibu wa kuwalinda raia wake dhidi ya Hamas na makundi mengine ya kigaidi na kuzuia mashambulizi ya siku za usoni.
Akizungumza na waandishi habari, Blinken amesema, amekubaliana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu mpango utakaowezesha misaada ya kibinadamu kuwafikia raia ndani ya Gaza.
Blinken aliyerudi Israel baada ya ziara katika baadhi ya mataifa ya Kiarabu kwenye kanda hiyo, alifanya mazungumzo ya zaidi ya saa sita na baraza la mawaziri la vita la Israel, hadi usiku wa manane.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na Blinken, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant alisema: "Hivi vitakuwa vita vya muda mrefu; gharama itakuwa kubwa. Lakini tutashinda kwa ajili ya Israeli na Wayahudi na kwa maadili ambayo nchi zote mbili (Israel na Marekani) zinaamini."
Hamas linawashikilia mateka 199
Jeshi la Israel limesema kundi la Hamas linawashikilia mateka takriban watu 200 katika ukanda wa Gaza. Idadi hiyo iliyoongezeka ya mateka, imejiri mnamo wakati Israel inajiandaa kutuma vikosi ndani ya operesheni Gaza kwa lengo la kuliangamiza kundi la Hamas ambalo Ujerumani, Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa mengine yameliorodhesha miongoni mwa makundi ya kigaidi.
Daniel Hagari, ambaye ni msemaji wa jeshi la Israel amesema familia za watu wanaoshikiliwa mateka zimepewa taarifa. Watu hao walishikwa mateka wakati wanamgambo wa Hamas walipofanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7.
Hagari amesema juhudi kwa ajili ya wanaoshikiliwa mateka ni kipaumbele cha juu kitaifa, na kwamba jeshi pamoja na taifa la Israel kwa jumla zinafanya juu chini usiku na mchana kuwarudisha nyumbani.
Hofu ya kutokea Mzozo wa kibinadamu
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu mzozo wa kibinadamu, na unatafuta njia ya kuhakikisha wahanga wa mazozo huo wanafikiwa kupitia kivuko cha kusini cha Rafah kinachouunganisha ukanda wa Gaza na Misri.
Shirika la Afya Duniani WHO limekusanya takriban tani 26 za misaada yenye thamani ya dola milioni 1.2 ambayo inapaswa kupelekwa Ukanda wa Gaza.
Mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Mashariki mwa Mediterrania Ahmed-Al-Mandhari amesema, punde tu mpaka wa Rafah utakapofunguliwa, watawasilisha misaada hiyo kuwasaidia wahanga.
Kulingana na WHO, miongoni mwa misaada hiyo ni pamoja na ndege moja iliyobeba shehena ya dawa na vifaa vya matibabu.
Hata hivyo, Mandhari amesisitiza kuwa misaada hiyo ni kidogo na haiwezi kukidhi mahitaji.
Juhudi za Kidiplomasia
Mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani nchini Yemen, Gerald Feirstein aliyezungumza na shirika la habari la DW kuhusu ushiriki wa Marekani kidiplomasia katika mgogoro huo amesema nchi yake inaweza kuwa mshirika muhimu katika kuwashinikiza Waisraeli kuepuka kusababisha vifo vingi vya Wapalestina wasio na hatia.
Feierstein aliyefanya kazi pia kama mwanadiplomasia nchini Israel na sasa anafanya kazi na shirika lisilo la serikali lililoko Washington DC, amesema Marekani inahusika kujaribu kuzuia wanamgambo wa Hezbollah na Iran kuingilia kati mzozo huo, huku ikielezea wasiwasi mkubwa wa hali ya kibinadamu ndani ya Gaza.
Feierstein amesema tangazo la Israel kwamba inaruhusu maji kuelekea kusini mwa Gaza na vilevile kampeni kabambe ya kidiplomasia ya kuwashirikisha Waisraeli na Wamisri kupata suluhisho la jinsi misaada inaweza kufikishwa Gaza, ni mifano tu ya juhudi za kidiplomasia za Marekani.
Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alirejea tena Israel Jumatatu baada ya ziara katika baadhi ya nchi za kiarabu katika kanda hiyo.
Ujerumani kupiga marufuku mtandao unaounga mkono Palestina
Hayo yakijiri, shirika la upelelezi wa ndani la Ujerumani, BND, limesema linafanya kazi kupiga marufuku uungwaji mkono wa harakati za kundi la wanamgambo la Hamas na kuharamisha mtandao wa Samidoun unaounga mkono Palestina.
Rais wa shirika hilo Thomas haldenwang ameliambia bunge la Ujerumani wakati wa kikao maalum jana Jumatatu kwamba wanafanya juhudi zote kutumia uwezo wote uliopo kuhakikisha utekelezaji wa hatua hizo haraka iwezekanavyo.
Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya angani Gaza tangu wanamgambo wa Hamas walipofanya uvamizi ndani ya Israel Oktoba 7.
Wizara ya Afya ya Gaza imesema inakadiria kuwa takriban Wapalestina 2,750 wameuawa na 9, 700 wamejeruhiwa.