Rais Barack Obama ziarani Asia na Pacific
22 Aprili 2014Miezi karibu sabaa baada ya kufutilia mbali ziara yake barani Asia kufuatia mzozo wa bajeti nchini mwake,kushindwa utawala wa Obama kuizuwia Russia isiimeze Crimea kumezidisha hofu za wale wanaohisi Marekani haina tena nia au azma ya kuendelea kuwa mhimili wa eneo la Asia na Pacific.
Maneno ni mepesi kutoa" anasema mtaalam wa sayansi ya siasa kutoka Philippines Ramon Casiple."Lakini washirika wa Marekani wanataka kujua watapata nini mambo yakifikia kiwango cha kutorejea nyuma?
Tangu rais Barack Obama alipotangaza mwaka 2011mpango wa kuimarisha ushirikiano tangu wa kijeshi.kidiplomasia mpaka wa kibiashara pamoja na washirika wake wa eneo la Asia na Pacific,hakuna kikubwa kilichoshuhudiwa .
Rais Barack Obama anawasili mjini Tokyo kesho jumatano-ziara ya kwanza ya rais wa Marekani katika nchi hiyo shirika barani Asia tangu ile iliyowahi kufanywa na Bill na Hillary Clinton mnamo mwaka 1996.Atakuwa rais wa kwanza wa Marekani aliyeko madarakani kuitembelea Malaysia tangu Lyndon Johnson mnamo mwaka 1966.Washirika mfano wa Korea ya kusini na Philippines vituo vyengine viwili vya ziara ya rais Barack Obama katika eneo la Asia na Pacific nazo pia zina hamu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usalama.
Lengo la ziara ya rais Obama
Washirika wa Marekani wanajiuliza kama zinaweza kutegemea uungaji mkono wa Marekani katika mgogoro wa kugombea ardhi pamoja na China.
"Lengo la Marekani ni kuzihakikishia nchi hizo kwamba Marekani imekuja ipo na itakuwa macho linaapohusika suala la masilahi pamoja na China na mataifa mengine..."anasema Koichi Nakano,ambae ni mhadhiri wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Sofia mjini Tokyo.
Mvutano unligubika eneo la kaskazini mashariki ya Asia kutokana na ugonvi wa kihistoria na madai ya kuania viisiwa vya Senkaku/Diayou katika ya Tokyo na Beijing pamoja pia na ule kati ya Tokyo na Korea ya kusini kuhusiana na visiwa vya Takeshima/Dokto vilivyoko karibu na bahari ya Japan.
Beijing na Seoul zakasirishwa
Leo asubuhi wabunge 150 wa Japan walimiminika kwa wingi katika eneo la ibada la Yasukuni na kusababisha hasira za serikali za mijini Beiojing na Seoul.Wabunge hao wa kihafiodhina wakishirikiana na waziri wa mambo ya ndani Yoshitaka Shindo walifanya ibada ya wafu katika hekalu hilo la Shinto kuwakumbuka wanajeshi milioni mbili na laki tano waliuwawa wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman