Rais Alpha Conde apuuza shutuma za kuwaandama wapinzani
17 Novemba 2020Rais wa Guinea, Alpha Conde amezipuuza shutuma zilizotolewa na viongozi wa upinzani kwamba anawawinda na kuwanyanyasa. Conde amezungumza kwa mara ya kwanza katika mahojiano tangu alipochaguliwa tena kuliongoza taifa hilo kwa muhula wa tatu, katika uchaguzi uliokuwa na utata. Katika mahojiano yake na shirika habari la Ufaransa, AFP na kituo cha utangazaji cha Ufaransa RFI, Conde amesema hakuna mtu anayelengwa, isipokuwa tu watu wanaotuhumiwa kwa kusababisha ghasia kutokana na uchaguzi wa Oktoba 18.
Wanaharakati watano wa upinzani wameshtakiwa kwa kutoa vitisho vinavyoweza kuvuruga usalama na utulivu wa umma. Baada ya Conde kutangaza atagombea tena, hatua hiyo ilizusha maandamano na ghasia zilizosababisha kuuawa kwa watu kadhaa, wengi wao wakiwa raia. Huku waangalizi wa nchi za Afrika wakiunga mkono matokeo ya uchaguzi, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na Marekani zimeyatilia shaka matokeo hayo. Conde amezirudisha shutuma hizo kwa wapinzani, akiwalaumu kwa kusababisha machafuko nchini humo.