Raia wa Syria wafanikisha kutiwa mbaroni mtuhumiwa wa ugaidi
11 Oktoba 2016Hatua ya kukamatwa kwa raia huyo wa Syria Jaber Albakri imehitimisha takribani siku mbili za msako wa nchi nzima uliokuwa na lengo la kumtia mbaroni baada ya maafisa wa polisi kukuta vifaa vya miripuko pamoja na vifaa vingine vilivyokuwa vimefichwa katika nyumba moja kwenye mji wa mashariki wa Chemnitz nchini Ujerumani Jumamosi iliyopita.
Albakir ni miongoni mwa wahamiaji 890,000 waliowasili nchini Ujerumani mwaka jana kwa lengo la kutafuta hifadhi. Mkuu wa polisi wa jimbo la Saxony nchini Ujerumani Joerg Michaelis alisema kuwa raia watatu wa Syria waliomkamata mtuhumiwa huyo walimtambua kupitia picha zilizosambazwa na polisi katika mitandao ya kijamii ikiwa ni moja wapo ya juhudi za kufanikisha kumtia mbaroni.
Baada ya kufanikiwa kumfikisha katika makazi yao usiku wa Jumapili iliyopita , wawili miongoni mwao walimdhibiti Albakr huku mmoja wao akienda kutoa taarifa polisi pamoja na picha ya mtuhumiwa huyo iliyokuwa katika simu na hatimaye polisi kumtia mbaroni.
Ahusishwa na kundi la Dola la Kiisilamu
Waendesha mashitaka pamoja na polisi nchini Ujerumani wanasema wanamshuku Albakr kama mwanajihadi ambaye anamahusiano na kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu.
Idara ya ujasusi wa ndani nchini Ujerumani wamekuwa wakimsaka mtuhumiwa huyo tangu mwezi Septemba mwaka huu na waliziarifu mamlaka husika za jimbo la Saxony ijumaa iliyopita wakimhusisha na mipango ya shambulizi la kigaidi.
Wakati maafisa wapolisi walipofanya msako jumamosi iliyopita katika makazi yake yaliyoko katika mji wa Chemnitz ambako alidaiwa kuwa alikuwa akiishi, Albakr alifanikiwa kutoroka. Hata hivyo polisi walikuta ndani ya nyumba hiyo kilo 1.5 ya vifaa vya miripuko pamoja na vifaa vingine vya hatari. Mkuu wa makosa ya jinai Michaelis alisema kutokana na uchunguzi uliokwishafanyika hadi sasa tabia na mienendo ya mtuhumiwa huyo inaashiria kuwa ana mahusiano na kundi la ikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu ingawa afisa huyo hakuelezea kwa undani zaidi.
Afisa mmoja wa usalama nchini Ujerumani alisema hakujawa na ushahidi unaoonyesha kuwa Albakr amekuwa akipokea maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa kundi hilo linalojiita Dola la Kiisilamu ingawa afisa huyo ambaye hakutaka kueleza zaidi huku pia akikataa kutaja jina lake kwa sababu siyo msemaji rasmi wa suala hilo alisema bado wanaunganisha taarifa za uchunguzi walizo nazo ili waweze kutoa taarifa kamili.
Bado haijulikani jinsi alivyokutana na raia hao wa tatu wa Syria
Polisi wanasema ilikuwa bado hajajulikana wazi ni lini na ni kwa jinsi gani raia hao watatu wa Syria walikutana na mtuhumiwa huyo katika mji wa Leipzig ambao uko takribani kilomita 80 kutoka mji wa Chemnitz, au kama walikuwa tayari wakimfahamu huku polisi wakisema hawatatoa taarifa zaidi zinazohusiana na raia hao watatu wa Syria waliofanikisha kutiwa mbaroni kwa mtuhumiwa huyo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa polisi iwapo kutakuwa na viashiria vinavyoonesha kuwa mtuhumiwa huyo ana rekodi ya kuwa mfuasi wa makundi ya itikadi kali basi watu hao waliotoa taarifa zilizofanikisha kukamatwa kwake nao pia watakuwa hatarini.
Kwa upande mwingine waendesha mashitaka wanaohusika na kudhibiti matukio ya kigaidi nchini Ujerumani wamesema hapo jana kuwa hawakuweza kubaini kama kulikuwa kuna eneo maalumu lililokuwa limepangwa tayari kwa ajili ya kufanyika shambulizi.
Mwandishi : Isaac Gamba/ APE
Mhariri : Yusra Buwayhid