1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa kigeni wanashambuliwa Afrika Kusini

16 Aprili 2015

Chama tawala nchini Afrika Kusini African National Congress ANC kimelaani wimbi la mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni ambayo yamesababisha vifo vya watu sita na kusababisha hali ya wasiwasi nchini humo

https://p.dw.com/p/1F9DG
Picha: Reuters/R. Ward

Taarifa kutoka kwa chama cha ANC imesema katika kipindi cha majuma kadhaa sasa, taifa la Afrika Kusini limeghubikwa na wimbi la mashambulizi ya kufedhehesha yanayowalenga raia wa kigeni kutoka nchi nyingine za Afrika.

ANC imeyataja mashambulizi hayo vitendo vya kihalifu dhidi ya watu wanyonge ambao wanatafuta hifadhi, faraja na kujiendeleza kiuchumi na kuongeza raia wa kigeni hapaswi kulaumiwa kwa changamoto zinazowakumba raia wa Afrika Kusini.

Katika mji wa kusini mwa nchi hiyo wa Durban mashambulizi yaliyochochewa na chuki dhidi ya wageni yamezilenga biashara na makaazi ya raia wa kigeni wakiwemo kutoka Somalia, Ethiopia na Malawi licha ya polisi kuimarisha doria katika mji huo kuzuia mashambulizi hayo.

Rais yuko kimya

Taarifa hiyo kutoka kwa ANC inakuja baada ya shutuma kuwa Rais Jacob Zuma ameshindwa kutoa tamko hadharani kuyalaani mashambulizi hayo. Mapema mwaka huu, raia wa kigeni pia walishambuliwa na maduka yao kuporwa katika kitongoji cha Soweto kilichoko karibu na mji wa Johannesburg.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: AFP/Getty Images/R. Bosch

Mashirika ya kutoa misaada yamesema zaidi ya raia 2,000 wa kigeni wameutoroka mji wa Durban wakihofia maisha yao na sasa wanaishi katika kambi za muda chini ya ulinzi wa polisi na iwapo mashambulizi hayo hayatasitishwa,idadi ya waathiriwa inatarajiwa kuongezeka.

Mhamiaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Johnny ambaye ni raia wa Zimbabwe anasema anatafakari kurejea nyumbani

Jana maduka mengi yalifungwa katikati mwa mji wa Johannesburg baada ya wafanyaibishara kuhofia ghasia zitazuka baada ya vitisho kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

Msumbiji imetangaza inapanga kuwasaidia raia wake walioko Afrika Kusini kurejea nyumbani baada ya waziri wa habari wa Malawi Kondwani Nankhumwa kusema wanawarejsha nyumbani raia wao 400 waliochomewa nyumba na mali zao. Malawi ndiyo nchi ya kwanza ya Afrika kuwaondoa raia wake kutoka Afrika Kusini.

Mfalme anashutumiwa kuchochea chuki

Mfalme Goodwill Zwelithini kiongozi wa kabila kubwa zaidi nchini Afrika Kusini la kwa Zulu Natal anashutumiwa kwa kuchochea mashambulizi hayo baada ya kutoa hotuba wiki mbili zilizopita akiwataka raia wa kigeni kufunga virago na kurejea makwao.

Baadhi ya waafrika Kusini wakikabiliana na raia wa kigeni mjini Durban
Baadhi ya waafrika Kusini wakikabiliana na raia wa kigeni mjini DurbanPicha: Reuters/R. Ward

Mwakilishi wa mfalme huyo Thulani Zulu amekanusha kuwa mfalme huyo ndiye aliyechochea mashambulizi hayo na kuongeza kuwa amesikitishwa na yanayojiri na anayalaani .

Wanaharakati wanaopinga chuki dhidi ya raia wa kigeni wanapanga maandamano makubwa mjini Durban hii leo kuishinikiza serikali kuchukua hatua zaidi kuwalinda wahamiaji. Polisi Afrika Kusini imesema imewakamata watu74 kuhusiana na mashambulizi hayo.

Raia wa Afrika Kusini ambao hawana ajira wanawashutumu wageni kuwa wanachukua nafasi zao za kazi. Mwaka 2008, watu 62 waliuawa katika mitaa ya Johannesburg kutokana na chuki hizo dhidi ya wageni.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman