Qatar yaendelea kusaka suluhu ya Gaza
21 Juni 2024Matangazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, yuko ziarani mjini Madrid na amezungumza na mwenzake wa Uhispania, José Manuel Albares ambaye amesema wameafikiana kikamilifu kwamba amani ya haki na ya kudumu inaweza kupatikana tu ikiwa kutakuwepo suluhisho la mataifa mawili na kupatikana kwa taifa halisi la Palestina.
"Kwa hiyo tunapigia upatu kufanyika kwa mkutano wa amani utakaozijumuisha pande zote mbili pamoja na jumuiya ya kimataifa." Alisema Albares.
Qatar, Marekani na Misri, zimekuwa katika mazungumzo ya upatanishi kwa miezi kadhaa, lakini hadi sasa walifanikiwa tu kupata usitishwaji mapigano wa siku saba mwezi Novemba mwaka jana, ambayo yaliwezesha kuachiliwa kwa mateka zaidi ya 100.