Qatar wapiga kura ya bunge
2 Oktoba 2021Wapigakura waliingia vituoni wakitenganishwa wanawake na wanaume mbali, kuwachaguwa wajumbe 30 kati ya 45 wa chombo kiitwacho Baraza la Shuraa, ambapo nafasi 15 zilizosalia zitajwa kwa uteuzi utakaofanywa na mtawala wa taifa hilo, afahamikaye kama amiri.
"Kwa fursa hii ya kupiga kura, nahisi kwetu ni ukurasa mpya," mwandishi wa vitabu vya watoto aliyetaka atambuliwe kwa jina moja tu la Munira aliliambia shirika la habari la Reuters baada ya kupiga kura yake mjini Doha, akiongoza kwamba: "Nimeifurahia kwelikweli idadi ya wanawake wanaowania nafasi kwenye uchaguzi huu."
Baraza la Shuraa litakuwa na mamlaka ya kibunge, yakiwemo ya kuidhinisha sera kuu za taifa na bajeti.
Bunge lisiloidhibiti serikali
Hata hivyo, Baraza hilo halitakuwa na udhibiti kwa baraza la mawaziri, ambalo ndilo linalotunga sera za ulinzi, usalama, uchumi na uwekezaji kwa taifa hilo dogo na tajiri kwa uzalishaji wa mafuta, ambalo limepiga marufuku vyama vya kisiasa.
Orodha iliyotolewa na serikali inaonesha kuwa katika wagombea 234 wanaowania uwakilishi wa wilaya 30 za nchi hiyo, 26 ni wanawake.
Kwa muda mrefu, Qatar imekuwa ikifanya chaguzi za mabaraza ya miji, lakini uchaguzi wa leo wa bunge ni wa kwanza na wa aina yake, ambapo wagombea walijinadi kupitia mitandao ya kijamii, mikutano ya hadhara na mabango ya barabarani.
Kutanuka kwa demokrasia
"Huu ni uzoefu wa mara ya kwanza kwangu... kuwa hapa na kukutana na watu kuzungumzia mambo haya tunayoyahitaji," alisema Khalid Al Mutawah anayewania wilaya ya Markhiya.
"Kufikia jioni ya leo, watu wa Qatar watajikuta wamekuwa sehemu ya ufanyaji maamuzi," alisema mgombea mwengine mwanamme kwenye wilaya hiyo hiyo, Sabaan Al Jassim mwenye umri wa miaka 65.
Kwa mujibu wa Allen Fromherz, mkurugenzi wa Kituo cha Masomo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Georgia, kura hii inaonesha jinsi ambavyo familia ya Al Thani inayotawala Qatar "inavyolichukulia kwa umakini suala la ugawanaji madaraka kwa ufanisi pamoja na makundi mengine ya kikabila ya Qatar."
Uchaguzi huu, ambao ulipitishwa kwenye kura ya maoni ya katiba ya mwaka 2003, unafanyika wakati Qatar ikijiandaa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Dunia hapo mwakani.