Pyongyang yarusha makombora katika visiwa vya Korea Kusini
5 Januari 2024Mabadilishano hayo yamesababisha wakaazi katika visiwa viwili vya ndani vya Korea Kusini kwenye mpaka wa magharibi wa baharini kukimbilia kwenye maeneo salama ya kukinga mabomu kufuatia maelekezo ya jeshi la Korea Kusini, kabla ya jeshi hilo kufyatua risasi za moto kuelekea mstari wa kikomo wa kaskazini katika eneo linalozozaniwa.
Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Korea Kusini Lee Sung-joon, makombora yote ya Korea Kaskazini yalitua upande wa kaskazini wa mpaka wa bahari na kuongeza kuwa jeshi la Seoul limekuwa likifuatilia nyendo za jirani yake Pyongyang katika pwani zake kwa kushirikiana na jeshi la Marekani.
"Tarehe 5, Korea Kaskazini ilifyatua makombora zaidi ya 200 kutoka saa tatu hadi saa tano asubuhi katika maeneo ya Jangsangot katika sehemu ya kaskazini ya Kisiwa cha Baengnyeong na Deungsangot katika maeneo ya kaskazini ya Kisiwa cha Yeonpyeong. Hapakuwa na madhara kwa raia au jeshi, na mahali palipoathirika ni eneo la kaskazini la mstari wa kikomo," alisema Sung-joon.
Waziri wa ulinzi wa Korea Kusini Shin Won-sik ameitaja hatua hiyo ya Pyongyang kuwa "ni kitendo cha kichokozi kinachochochea mvutano na kutishia amani katika rasi ya Korea".
China ambayo ni mshirika mkuu wa kisiasa wa Korea Kaskazini, imetoa wito kwa pande zote kujizuia na kuzitaka nchi hizo mbili kurejea katika mazungumzo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Wang Wenbin amewaambia waandishi wa habari kuwa, kutokana na hali ya sasa Beijing inatumai kuwa pande zote mbili zitaendelea kuwa tulivu na kujiepusha kuchukua hatua ambazo huenda zikazidisha wasiwasi.
Soma habari inayohusiana na taarifa hii: Korea Kaskazini kupeleka jeshi mpakani mwa Korea Kusini
Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano mkuu wa chama wiki iliyopita, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alisema kuwa kuwa suala la kuungana na Korea Kusini haliwezekani kabisa na kwamba Pyongyang inabadili sera zake kuelekea jirani yake huyo wa Kusini inayomchukulia sasa kama adui.
Soma kauli ya kiongozi wa Korea Kaskazini: Kim Jong Un aamuru jeshi 'kuziangamiza kabisa' Marekani, Korea Kusini iwapo watachokozwa
Eneo la baharini karibu na mahali panapozozaniwa pamekuwa kitovu cha mapigano mabaya baina ya nchi hizo mbili ikiwemo vita vilivyohusisha meli za kivita na kuzama kwa meli ndogo ya kivita ya Korea Kusini mwaka 2010 katika kile kinaaminika kuwa ni shambulizi lililofanywa na Korea Kaskazini na kuwaua mabaharia 46.
Uhusiano baina ya nchi mbili za Korea kwa hivi sasa umedorora baada ya Kim kuiweka hadhi ya nchi hiyo kuwa yenye nguvu za nyuklia katika katiba wakati akifanya majaribio ya makombora ya masafa marefu.