1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin 'sio mshukiwa pekee' katika uhalifu nchini Ukraine

9 Novemba 2022

Bunge la Ukraine limeitaka jumuiya ya kimataifa kuanzisha mahakama maalum ya kimataifa kwa ajili ya uhalifu wa uvamizi uliofanywa na Urusi dhidi ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4JGbw
Russland Tag der nationalen Einheit | Präsident Putin in Moskau
Picha: Mikhail Metzel/Sputnik/REUTERS

Katika mahojiano na DW, Claus Kress, mtaalamu wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cologne nchini Ujerumani, anaeleza jinsi mahakama kama hiyo inaweza kufanya kazi na kwa nini haihitaji ridhaa ya Urusi, huku akibainisha kuwa hukumu ya Rais Vladimir Putin si lazima.

Universität Köln l Prof. Dr. Claus Kreß
Profesa Claus Kress wa Chuo Kikuu cha ColognePicha: Pascal Buenning

Claus Kress wa Chuo Kikuu cha Cologne ameiambia DW  kuwa kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kimataifa ya kujaribu kuchunguza uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine itakuwa ishara muhimu, hata kama hakutakuwa na hukumu itakayotolewa.

Kress amesema mahakama hiyo maalum ingeshughulikia shtaka la uvamizi. Hilo ni muhimu sana kwa Ukraine kwa sababu linahusu shutuma za vita. Kwa mtazamo unaoeleweka wa Ukraine, kuanzisha vita vya uchokozi ni "kosa kubwa" ambalo limekuwa likisababisha ukatili unaofanywa wakati wa vita, ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita.

Soma zaidi:Ukraine yaapa kutoiachia Urusi hata sentimita moja mashariki 

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo nchini Ujerumani, Kress amesema Ujerumani, sambamba na mataifa mengine, bado hayajadhihirisha azma hiyo, kutokana na ukweli kwamba kuna masuala magumu ya kisheria na kisiasa yanayopaswa kutathminiwa. Kress amebainisha kuwa mazungumzo yamepiga hatua kubwa hivi karibuni, lakini hakujua ni lini yatakamilika.

 

Ni vipi mahakama hiyo maalum yaweza kuundwa?

Niederlande | Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, The Hague UholanziPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Kress amesema aina mbalimbali zinajadiliwa kwa sasa. Mfano unaopendekezwa una hatua mbili, ya kwanza ikiwa ni azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Kabla ya kuanzisha mchakato huo ni lazima kuwa na uhakika wa kupata idadi kubwa ya kura zinayohitajika. Tofauti na hivyo itakuwa ni jambo la kuhuzunisha kwa Ukraine, ikiwa kura kama hiyo itashindwa katika mkutano huo muhimu.

Soma zaidi:UN: Urusi imefanya mauaji ya kikatili nchini Ukraine 

Tofauti na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu haliwezi kuanzisha mahakama ya kimataifa ya uhalifu, lakini inaweza, kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, kutaja nia ya jumuiya ya kimataifa ya kufanya hivyo. Hilo lingekuwa na umuhimu mkubwa kuhusu uhalali wa mahakama hiyo. Kisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaweza kuhitimisha mkataba wa kimataifa na Ukraine juu ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Je, hilo lingechukua muda gani?

Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag
Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Kesi za jinai ni mchakato mgumu. Hatua ya kwanza inahusisha kuanzishwa kwa uchunguzi. Hii inamaanisha kupata ushahidi na ikiwa itathibitika, kuamua ni nani anayeshtakiwa na kutoa maelezo sahihi kuhusu tuhuma zinazomkabili. Huo pekee ni mchakato unaohitaji umakini wa hali ya juu.

Mtaalamu huyo wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cologne anasema uhalifu wa uvamizi umejikita katika ngao ya sheria za kimataifa, lakini hadi sasa kumekuwa na kesi chache mno za kimataifa.

Soma zaidi: Ukraine yataja masharti ya kufanya mazungumzo na Moscow

Hadi leo hii kesi katika mahakama za kijeshi huko Nuremberg na Tokyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia ndizo zinazotambulika. Kwa hivyo hatua yoyote ya kuanzisha tuhuma za uvamizi inabidi izingatiwe vyema na wala tusitarajie mchakato wa haraka wa kuanzishwa mahakama kama hiyo.

Hata hivyo, kitendo tu cha kuanzishwa kwa uchunguzi na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kungepeleka ujumbe muhimu kwamba jumuiya ya kimataifa inalichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa.

Je, vita inabidi viishe kabla ya kesi kuanza na nani mlengwa?

Russland, Kostroma | Reservisten der russischen Armee
Wanajeshi wa Urusi wakionekana kwa viatu vyao vya kijeshiPicha: /Russian Defence Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Kwa upande wa Mahakama za Nuremberg na Tokyo, lakini pia katika kesi nyingi zilizoshughulikiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kama kesi kuhusu Yugoslavia na Rwanda, nyakati mbaya zaidi za mzozo zilikuwa tayari zimefikia tamati, lakini kimsingi, kesi zinaweza kuanza hata kabla ya vita kumalizika. Hali ilibadilika baada ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC mwaka 2002. Mahakama hiyo ni taasisi ya kudumu na inaweza kuanzisha uchunguzi mara tu kunapoibuka tuhuma za uhalifu.

Soma zaidi: Ukraine inaandaa kesi kadhaa za uhalifu wa kivita

Claus Kress amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin, ndiye mshtakiwa mkuu, kwa mashtaka ya uhalifu wa uvamizi. Lakini Putin sio mshukiwa pekee. Kuhusu uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya halaiki, kwa kawaida kuna wahusika wakuu, lakini pia wale wanaohusika katika ngazi za chini za uongozi, na kisha wale wanaofanya ukatili huo kwenye maeneo ya mapigano. Tuhuma kama hizo hazielekezwi kwa mtu mmoja pekee.