Putin: Operesheni ya Ukraine haijapata mafanikio
12 Septemba 2023Matamshi hayo ameyatoa katika wakati anajitayarisha kwa mkutano na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ambao huenda utajumuisha Moscow kuomba silaha za kuendeleza vita nchini Ukraine.
Rais Putin leo alikuwa mwenyeji wa mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Mataifa ya Asia Mashariki huko kwenye mji wa Vladivostok.
Alizungumza kwa saa kadhaa ikijumuisha hotuba mbele ya washiriki na kipindi cha maswali na majibu pamoja na waandishi habari.
Aligusia masuala chungunzima tangu vita nchini Ukraine, hali ya uchumi wa Urusi, kuimarika kwa nafasi ya China mbele ya jukwaa la kimataifa pamoja na siasa za Marekani ikiwemo kizungumkuti kinachomkabili rais wa zamani wa taifa hilo Donald Trump anayeandamwa na kesi za jinai.
Kuhusu vita nchini Ukraine, kiongozi huyo wa Urusi ameyapinga madai ya Ukraine kwamba imeyakomboa maeneo kadhaa yaliyokuwa yakidhibitiwa na Urusi kupitia kampeni yake ya kujibu mapigo iliyoanza mwezi Juni.
Putin amesema licha ya tambo za serikali mjini Kyiv juu ya vikosi vyake kusonga mbele kwenye uwanja wa vita, ukweli wa mambo ni kwamba hakuna matokeo yoyote ambayo Ukraine imeyapata.
"Ukraine inaendesha kile kinachoitwa operesheni ya kujibu mapigo lakini hakuna matokeo yoyote, huo ndio ukweli. Hatuwezi kusema operesheni hiyo imegeuka fedheha au la, ila ni kwamba hakuna mafanikio. Kuna hasara kubwa. Tangu kuanza kwake, vifo vya wapiganaji ni 71,000". Amesema rais Putin.
Putin asema Urusi itaendelea na vita hadi Ukraine isalimu amri
Hata hivyo mtizamo huo ni tofauti na kile kinachoeelezwa na Ukraine na wachambuzi wengine wa vita. Pande hizo mbili zote zinasema vikosi vya Ukraine vinasogea mbele kwenye mkoa wa Zaporizhzhya na hata Donetsk.
Lakini kile kilicho na dhahiri ni kwamba kasi ya mapambano na kupata ushindi kwa vikosi vya Ukraine bado ni ndogo ikilinganishwa na livyotarajiwa hapo kabla.
Hata msemaji wa jeshi la Ukraine, Oleksandr Shtupun, aliarifu hapo siku ya Jumatatu kuwa vikosi vyao vinapiga hatua mbele ya angalau mita 50 hadi 200 kwa siku kwenye uwanja wa mapambano.
Kwenye matamshi yake Putin ameashiria kuwa ataendelea kupigana nchini Ukraine hadi pale vikosi vya Kyiv vitakaposalimu amri.
Amesema Urusi haitokuwa ya kwanza kusisimamisha mapigano wakati Ukraine bado ´inatunisha misuli´.
Je, msimamo wa Putin ndiyo ajenda kuu ya mkutano wake na Kim wa Korea Kaskazini?
Msimamo huo wa Putin yumkini ndiyo umeifanya Marekani kushuku kuwa mkutano wake unaotarajiwa muda wowote kutoka sasa na kiongozi wa Korea Kaskazini utatuama juu ya ajenda ya Moscow kujipatia silaha kutoka Pyongyang.
Kim Jong Un aliwasili Urusi mapema hii leo kwa mkutano wa historia kati yake na Putin ambao Washington inasema utajadili uwezekano wa Korea Kaskazini kuipatia Urusi silaha kwa ajili ya vita vya Ukraine.
Moscow kwa upande wake itatimiza matakwa ya Kim ya kuisaidia Korea Kaskazini kwa teknolojia ya kisasa ya satelaiti na uundaji nyambizi zinaendeshwa kwa nyuklia.
Hadi sasa haijafahamika ni wapi wawili hao watafanya mkutano wao lakini duru zinasema itakuwa ni upande wa mashariki mwa Urusi na hususani kwenye kituo cha anga za mbali cha Urusi huko Vostochny.