Putin kukutana na rais Erdogan juu ya mkoa wa Idlib
5 Machi 2020Viongozi wote wawili wameelezea matumaini ya kufikiwa makubaliano mapya ya kupunguza ongezeko la machafuko katika mji wa Idlib ambao ndio mji wa mwisho nchini Syria unaoshikiliwa na waasi. Rais Erdogan amesema anatazamia rais Putin atakubali usitishaji wa haraka wa mapigano mjini Idlib ambako, Ankara inapambana dhidi ya vikosi vya Syria vikiungwa mkono na Urusi.
"Ninatarajia kufanikisha usitishaji mapigano katika mkoa huo. Hii ndio ajenda yetu kubwa katika mazungumzo na Putin," alisema Erdogan.
Mapigano makali yamewaua askari kadhaa wa Uturuki mjini Idlib katika wiki za hivi karibuni, wakati Ankara kwa mara ya kwanza
ilipoanzisha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa rais Bashar al-Assad. Wiki iliyopita rais Erdogan aliyaeleza mataifa ya Ulaya kuunga mkono juhudi zake nchini Syria baada ya kufungua mpaka wa Uturuki na Ugiriki na kuibua mgogoro mpya wa wahamiaji na wakimbizi.
Uturuki kwa muda mrefu imekuwa ikiyaunga mkono baadhi ya makundi ya waasi dhidi ya Assad lakini kipaumbele chake kwa hivi sasa ni kukomesha wimbi jingine la wakimbizi, mnamo wakati raia karibu milioni moja mjini Idlib wakikosa makaazi kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Syria.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema kwamba viongozi hao wawili watajadili juu ya chanzo na athari za mzozo pamoja na "hatua za pamoja", wanazoweza kuafikiana kwa ajili ya kupunguza mvutano.
Lakini Moscow ambayo ilianzisha mashambulizi ya angani kumuunga mkono Assad mwaka 2015, itakuwa na lengo la kutuma ujumbe kwamba Uturuki haitoizuia Syria kuyatwaa tena maeneo yake. Kremlin inaitizama kampeni ya Urusi nchini Syria kama ushindi muhimu wa sera ya kigeni ya Putin na wachambuzi wanasema rais huyo hajaribu kukabiliana na mwanachama wa Jumuiya ya kujihami NATO yani Uturuki lakini pia hayuko tayari kurudisha nyuma majeshi yake.
Makubaliano ya awali yalivunjika kwa haraka. Uturuki na Urusi ambazo zinaunga mkono pande tofauti katika vita ya Syria, zimekuwa zikitupiana lawama kwa kushindwa kuheshimu makubaliano hayo.