Putin kubaki madarakani milele?
11 Machi 2020Bunge la nchi hiyo linatarajiwa leo kuidhinisha mapendekezo kadhaa ya mabadiliko, ikiwa ni pamoja na kumuwezesha rais Putin kugombea muhula mwingine madarakani.
Vladimir Putin alijitokeza katika bunge la Urusi jana Jumanne , wakati baraza hilo la wawakilishi likijadili mabadiliko hayo ya katiba. Katikati ya mwezi Januari Putin alianzisha kwa mshangao wa wengi mchakato huo wa mabadiliko ya katiba. Kutakuwa na mabadiliko mengi katika katiba ya nchi hiyo, kwa mfano mshahara wa kima cha chini.
Lakini kuhusu suala muhimu katika siasa za Urusi, ni vipi Urusi itaweza kujiendesha baada ya mwaka 2024, wakati muhula wa Putin madarakani utakapomalizika rasmi, kwa mpango huo hakuna jibu hadi sasa.
Kiongozi wa muda mrefu
Putin, mwenye umri wa miaka 67, amekuwa madarakani kama rais na baadaye waziri mkuu kwa miongo miwili. Ni kiongozi aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi nchini Urusi ama kiongozi wa Kisovieti tangu Joseph Stalin.
Katiba ya nchi hiyo katika hali yake ya sasa inaruhusu rais kutumikia kwa mihula miwili mfululizo, ikiwa na maana kwamba Putin ataondoka madarakani kama rais katika muda wa miaka minne ijayo. Putin alitumikia vipindi viwili vya miaka minne kama rais kuanzia mwaka 2000 hadi 2008. Baada ya katiba kufanyiwa mabadiliko kutoa ruhusa ya mihula ya miaka sita, na Putin alirudi kuwa rais mwaka 2012 na alichaguliwa tena mwaka 2018.
Baraza la wawakilishi
Baraza la wawakilishi la bunge la Urusi Duma linadhibitiwa na chama cha siasa ambacho kiko karibu zaidi na Putin, United Russia, ambacho kwa wingi mkubwa kinaunga mkono mswada mpya wa mabadiliko. Baada ya kupitishwa katika baraza la wawakilishi, mswada huo unatarajiwa kuidhinishwa na baraza la juu, seneti siku ya Jumamosi, na kisha utapelekwa katika mahakama ya katiba.
Putin angependa kutia saini kuwa sheria mswada huo hapo Machi 18, katika kumbukumbu ya kuchukuliwa jimbo la Ukraine la Crimea na kuingizwa katika himaya ya Urusi.
Putin amesisitiza kwamba mabadiliko hayo yaidhinishwe kupitia kura ya maoni nchi nzima hapo Aprili 22 ili kuanza kazi. Mabadiliko hayo ni pamoja na kuweka kima cha chini cha mshahara na fungu la mafao ya uzeeni kwa msingi wa gharama za maisha, kipengee ambacho kinaweza kusaidia wananchi kupiga kura kuidhinisha mabadiliko hayo.